HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 29, 2021

SERIKALI YAMALIZA MGOGORO ENEO LA UFUKONI STENDI MTWARA


Na Munir Shemweta, MTWARA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa Mtaa wa Ufukoni Stendi eneo la Libya mkoani Mtwara na Kampuni ya Azimio Estate na kuleta furaha kwa wananchi.

Mgogoro wa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 404 unahusisha takriban kaya mia tano zenye wakazi zaidi ya 1000 ulikuwa na kesi mara kadhaa na kuipa ushindi kampuni ya Azimio Estate jambo lililowafanya wakazi wa eneo hilo kuishi kwa hofu kwa muda wote.

Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula jana Julai 28, 2021 alifika eneo la mgogoro huo akiambatana na uongozi wa wilaya ya Mtwara, Mbunge wa jimbo la Mtwara, Diwani wa eneo hilo na wataalamu wa sekta ya ardhi kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo ulioelezwa kuwa umedumu kwa muda mrefu.

Akiwa katika eneo la tukio Dkt Mabula alisikiliza maelezo ya pande zote mbili wakiwemo wawakilishi wa kampuni ya Azimio Estate kwa lengo la kujua historia ya mgogoro na namna ya kumaliza mgogoro huo bila kuathiri upande wowote.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mgogoro huo Dkt Mabula alisema, Kampuni iliyonunua eneo hilo la shamba la chumvi ilinunua kwa mmiliki ambaye historia inaonesha halijawahi kulipiwa fidia kwa wamiliki wa awali wsakati wa kulichukua.

‘’Kwa sababu mmekubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia basi mkubali kupata mtakachopata katika eneo hili, eneo la chumvi litabaki kama lilivyo na eneo la makazi ya wananchi watarasimishiwa na hapa tunaangalia utu na maslahi ya taifa’’ alisema Dkt Mabula.

Alisema, maamuzi ya wizara ya ardhi kwenye mgogoro huo ni kuendelea na zoezi la urasimishaji kwa maeneo ya wananchi na mwekezaji atatakiwa kurudisha hati kwa ajili ya kupangwa upya na anatakaporudidha atatakiwa pia kulipa na kiasi cha shilingi milioni 34 ya kodi ya pango la ardhi anayodaiwa ambayo hakuilipwa kwa muda mrefu.  Na maeneo yaliyobaki wazi katika hati yatapimwa upya na kupewa mwekezaji na wananchi wataachiwa maeneo wanayomiliki sasa.

‘’Hata wewe hutakuwa na amani kung’ang’ani eneo ambalo kila mmoja ana kinyongo hata kazi yako haiwezi kwenda vizuri na eneo lililobaki ni kubwa zaidi kuliko la wananchi na tunachokifanya ni kungalia utu mbele lakini pia na maslahi ya taifa ambacho kitu kikubwa ni wananchi kuishi kwa amani na utulivi’’ alisema Dkt Mabula.

Aliwataka wananchi wa eneo hilo la Ufukoni wakati zoezi la kuanisha maeneo likiendelea basi wawe watulivu na kutoa ushirikiano ili kuweza kumaliza tatizo hilo kwa amani na kuweza kusonga mbele.

Awali wananchi wa eneo hilo walieleza kuwa, eneo hilo lenye mgogoro baina yao na kampuni ya Azimio Estate ni  la kwao kwa kuwa walirithi kutoka kwa mababu zao na wanashangaa kuambiwa kuwa ni wavamizi jambo walilolieleza kuwa limekuwa likiwatia hofu kiasi cha baaadhi yao kupoteza maisha.

Walimuomba Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula kuwasaidia kumaliza mgogogoro huo na kurasimishiwa makazi yao ili waweze kuishi kwa amani na familia zao.

Eneo lenye mgogoro la Ufukoni Stendi mkoani Mtwara lina ukubwa wa ekari 404 na lilikuwa likimilikiwa na Shirika la Mtwara Development Cooperation Limited (MTWADECO) ambapo mwaka 2000 waliokuwa wafanyakzi wa Shirika hilo walifungua kesi Mahakamni kulalamikia kutolipwa stahiki na mahakama iliamuru liuzwe na wadai kulipwa stahiki zao

Kwa mara kadhaa eneo hilo limehamishwa umiliki kutoka MTWADEKO kwenda kwa Abdallah Ismail naye alihamisha umiliki kwenda kwa Intergrated Cement Co Ltd kabla ya kwenda kwa   Abdulrahmani Sinani ambaye naye alihamisha miliki kwa Azimio Housing Estate.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakazi wa mtaa wa Ufukoni Stendi mkoani Mtwara alipokwenda kutafuta suluhu ya mgogoro wa eneo hilo kati ya wananchi na kampuni ya Azimio Estate Ltd .
Mkazi wa mtaa wa Ufukoni Stendi mkoani Mtwara Ahmad Chapchap akiwasilisha malalamiko yake kuhusiana na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa mtaa huo na kampuni ya Azimio Estate.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili mtaa wa Ufukoni Stendi mkoani Mtwara kutafuta suluhu ya mgogoro wa eneo hilo kati ya wakazi wa eneo hilo na kampuni ya Azimio Estate Ltd.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad