Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini(RITA) Umewataka wanafunzi wanaofanya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo ili kupata mikopo ya elimu ya juu kuzingatia hatua za uhakiki huo.
Akizungumza leo Julai 28,2021 kutoka kwenye banda la RITA katika maonyesho ya 16 ya Elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia, Ofisa Habari wa RITA, Grace Kyasi amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosea hatua za kutuma maombi yao ya uhakiki wa vyeti.
Ambapo wamekuwa wakitumia njia ya barua pepe ya Wakala ambayo ni info@rita.go.tz badala ya kutuma maombi yao kupitia ukurasa wa huduma mtandaoni unaojulikana kama E-huduma ambapo mwanafunzi anatakiwa aingie kwenye tovuti ya www.rita.go.tz na kisha aingie kwenye kipengele cha E-huduma ili kutuma taarifa zake.
Grace amesema kuwa ili maombi ya uhakiki wa vyeti vya mwanafunzi yapokelewe na kufanyiwa kazi kwa ufasaha, mwanafunzi anatakiwa ajisajili kwa kujitengenezea akaunti yake katika ukurasa wa RITA huduma mtandaoni na kisha kuingia katika kipengele cha uhakiki na kutuma maombi ya taarifa zake ili ziweze kushughulikiwa na kujibiwa kwa wakati.
Aidha amesema mpaka sasa tayari jumla ya maombi 84,387 yameshahakikiwa na kurudishwa kwa wanafunzi ili kuweza kuendelea na utaratibu wa kuomba mikopo katika ofisi ya Bodi ya mikopo elimu ya juu.
"Pia tunapenda kuwakumbusha wanafunzi kutumia simu yetu ya huduma kwa wateja ambayo ni 800117482 iwapo watahisi kupata changamoto yoyote katika utumaji wa maombi yao ya uhakiki." amesema na kuongeza RITA umeshiriki katika maonyesho ya 16 ya Elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU) yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Amesema kaatika maonyesho hayo RITA inatoa huduma ya Usajili wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na Elimu kwa Umma kuhusu huduma ya Vizazi,Vifo,Ndoa,Talaka,Udhamini,Ufilisi, Wosia na Mirathi hivyo wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la RITA ili kufaidika na huduma hizo mahususi.
Mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa maonyesho hayo yaliyoanza tangu tarehe 26 na kutarajiwa kuhitimishwa tarehe 31 Julai alikuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Zena Ahmed Said.Afisa habari kutoka RITA, Bi. Grace Kyasi akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la RITA katika Maonesho ya 16 ya Elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Ilala leo.
Wananchi wakipata huduma mbalimbali katika banda la RITA viwanja vya mnazi mmoja leo.
No comments:
Post a Comment