HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 20, 2021

MIGOGORO YA NDOA NA TALAKA HOLELA MWIBA NDANI YA JAMII- MIKULU

 Na Mwamvua Mwinyi, RUFIJI

MIGOGORO ya ndoa,talaka holela katika baadhi ya maeneo wilaya ya Kibiti ,mkoani Pwani inadaiwa kuwa mwiba katika familia , hali inayotajwa kusababishwa na kuingia katika ndoa kwenye umri mdogo na kukosa elimu ya ndoa .

Aidha uaminifu kwa wana ndoa umekuwa haba na kusababisha kutokea kwa migogoro hiyo na kuleteana magonjwa ikiwemo ya zinaa na maambukizi mapya ya VVU.

Afisa ustawi wa jamii kituo cha afya huko Kibiti ,Hadija Msuya pamona na Mratibu wa asasi inayoshugulikia masuala ya msaada wa kisheria kutoka JICHO ANGAVU FOUNDATION, Hussein Mikulu walisema ,ndoa nyingi hazipati elimu ya masuala ya ndoa na kutegemea mafundo ya kitchen party.

Hayo waliyasema baada ya mkutano ulioandaliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC),ambao uliwakutanisha wadau watatu wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ,waandishi wa habari na idara za serikali ,kujadili namna ya kutatua migogoro ndani ya jamii kupitia njia ya ushirikishwaji kwa amani na kutafuta mbinu za kuleta utatuzi,mkutano uliofanyika Rufiji mkoani Pwani.

Walisema ,wamekuwa wakipokea malalamiko zaidi ya 20 kwa mwezi kuhusiana na migogoro ya ndoa ,mirathi na migawanyo ya mali .

"Migogoro hii naweza sema imeshika kasi kutokana na ndoa nyingi kufungwa pasipo kupatiwa elimu za ndoa ,kuoana umri mdogo ,mmoja wa wanandoa kujiingiza kwa kufuata mali bila kuwa na utayari ,ushawishi wa familia na umasikini " alifafanua Hussein.

Hussein alibainisha ,matokeo ya kukosa uaminifu ni wivu wa mapenzi na baadae kusababisha migongano na hatimae kuachana na wengine kupigana hadi kujeruhiana,kuachiana ulemavu ama kuuwana (vifo ).


"Hilo ni tokeo moja ,pia kurudishana nyuma kimaendeleo ,kuwasababishia watoto kukosa matunzo bora ,kuanza utoro na kukatisha masomo ,watoto kuwa yatima mmoja wapo akifariki na baadhi ya watoto hujiingiza katika ajira za utotoni na watoto wa kike kupata mimba za utotoni "

Nae afisa ustawi wa jamii kituo cha afya Kibiti, Hadija alisema ,wamekuwa wakipokea kesi za wanandoa kutelekezwa, kukosa matunzo na kupeana talaka holela bila kufuata misingi ya ndoa.

Hadija alisema, kikubwa wao husaidia kusuluhisha ili kurudisha amani na kukumbusha jamii kuwa jukumu la kulea familia sio la mwanamke pekee ,jukumu la kulea ni la pande zote mbili kwani ukikuta upande mmoja hauwajibiki ndipo tatizo linapoanzia.

Kwa upande wake ,mkazi wa Kibiti ,Mariam Mkundi (38) alisema ,aliolewa na kuzaa mtoto mmoja na mumewe Abdallah Kigunda (45), lakini baada ya miaka mitatu ndoa ikaingia shubiri.

Alisema mgogoro ulipozidi ,alipewa talaka na mume kuanzia hapo hakujali familia wala kulea mtoto wao ambae kwasasa ana miaka mitano.

Mariam anadai alipeleka malalamiko ustawi wa jamii kituo cha afya Kibiti ,ambako walifuata taratibu za kumwita mlalamikiwa ambapo alifika na kuanzia sasa ametakiwa kutoa matunzo ya mtoto sh .30,000 kila mwezi.

Dawati la jinsia Kibiti, afande Sara alisema ,ufumbuzi wa migogoro hii ni kuendelea kutoa elimu inayohusiana na masuala ya ndoa kwa kushirikiana viongozi wa dini ,asasi za kiraia na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake ,sheikh mkuu wa mkoa wa Pwani ,Hamis Mtupa alisema dhana ya talaka maana yake ni utaratibu wa kuvunja mkataba wa ndoa baina ya wanandoa mbele ya mashahidi wawili kwa kuzingatia sheria ya kiislamu.

Alisema ,talaka sio jambo la masihala kama baadhi wanavyolichukulia ,kwani sio jambo linalompendeza allah ila linaruhusiwa pale inapobidi .

Mratibu wa mradi wa jenga amani yetu kutoka LHRC ,Caroline Shoo alisema wanatoa elimu na kufanya mikutano kukutanisha wadau hao kwa kushirikiana na shirika la Search for Common Ground na ZLC kwa ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya.

Caroline alieleza endapo migogoro midogo, ikiwemo ya ardhi ,wakulima na wafugaji pamoja na ndoa haipati suluhu kikamilifu basi hugeuka kuwa mikubwa na kufikia hatua ya kuvunja amani.

Aliiasa jamii kuheshimiana na kufuata sheria za nchi ikiwa ni sambamba na mamlaka husika kusimamia sheria na kutenda haki ili kupunguza migogoro hiyo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad