NA YEREMIAS NGERANGERA…NAMTUMBO
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Julius Ningu ameupongeza uongozi wa kata ya ligera kwa kuhamasisha wananchi wa kata hiyo kutumia nguvu zao kuanzisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike ili kupunguza adha ya wanafunzi hao kutembea umbali mrefu kuhudhuria masomo .
Akiongea na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa shule ya Sekondari , wajumbe wa kamati ya maendeleo ya kata, walimu wa shule ya sekondari Lukimwa pamoja na watendaji wa vijiji wa kata hiyo Mkuu wa wilaya hiyo aliwapongeza kwa jitihada ya kuhamasisha wananchi juu ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Lukimwa.
Aidha Ningu alidai ipo haja ya viongozi kushirikiana ,kushikamana na kuwa na hoja ya pamoja ya kusimamia shughuli za maelendeleo na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha zinazotumika ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuibuka .
Diwani wa kata ya Ligera bwana Sambode Mhongo alimhakikishia mkuu wa wilaya hiyo kuwa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Lukimwa uliibuliwa kwenye kikao cha maendeleo ya kata hivyo ushirikishwaji wa viongozi na wananchi ni mkubwa ,uwazi wa matumizi ya fedha nao ni mkubwa .
Pamoja na mambo mengine Mhongo alisema wananchi kwa uwezo wao kupitia vikao vya kisheria maendeleo ya kata walisema wapo tayari kujenga bweni hilo kwa kutumia nguvu zao mpaka hatua ya boma lakini pamoja na maamuzi hayo akaomba pia watu wenye mapaenzi mema ya kuunga juhudi zinazofanywa na wananchi hao kuchangia juhudi hio .
Kaimu mkuu wa shule ya sekondari Lukimwa bwana Kassian Lwehela alimwambia mkuu wa wilaya ya Namtumbo kuwa ushirikishwaji wa viongozi ,wananchi katika maswala yote yanayohusu shule hiyo ni mkubwa kwani kila jambo linaloamliwa katika vikao mihutasari ya vikao huandikwa na huwekwa kwa kumbukumbu alisema Lwehela.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo alifanya ziara ya kikazi katika shule ya sekondari ya Lukimwa kukagua utendaji kazi ,usimamizi wa miradi ya ujenzi wa maabara , bweni pamoja na kusikiliza changamoto zinazoikabili shule hiyo na kuzitafutia ufumbuzi huku akiwapongeza kwa kuanzisha ujenzi wa bweni la wasichana wa shule hiyo .
No comments:
Post a Comment