*Serikali yaeleza kutotegemea viongozi kwenda kinyume na maadili na haki baada ya mafunzo hayo
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
WAZIRI wa nchi, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohammed Mchengerwa amesema kuwa viongozi wote walioteuliwa wakiwemo wakuu wa Mikoa, Wilaya pamoja na Wakurugenzi lazima wapitie mafunzo wa Uongozi yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) taasisi ambayo imekuwa ikiwaandaa na kuwapika viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki, maadili na weledi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizundua bodi ya tatu ya wakurugenzi ya Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute,) Waziri Mchengerwa amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo hayo kwa viongozi wote wa Umma wakiwemo wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi, wakurugenzi wa Wizara, viongozi walioteuliwa na Mawaziri kupata programu za mafunzo maalumu ya uongozi kutoka Taasisi ya Uongozi ambayo imerejesha sifa ya kupika viongozi.
'' Ili watendaji wafanye kazi kwa weledi katika nafasi zao walizoteuliwa na wanazozitumikia wakiwemo vijana lazima wapite katika mikono ya Taasisi ya Uongozi ili watumikie nafasi zao kwa kuzingatia maadili, haki na weledi.'' Amesema.
Waziri Mchengerwa amesema, Hakuna kiongozi yeyote wa Umma na kuteuliwa ambaye hawatapitia mafunzo hayo na hawategemei baada ya mafunzo hayo viongozi hao kwenda kinyume na haki na maadili wa uongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pia amesema, Bodi ya wakurugenzi wa Taasisi ya Uongozi iliyozinduliwa leo imesheheni wataalamu wa elimu na viongozi wabobevu ambao watashirikiana na Taasisi hiyo ambayo Serikali inatambua mchango wake wa kuikuza Taasisi ya Uongozi ndani na nje ya nchi.
kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute,) na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,) Dkt. Stergomena Tax amesema, bodi mpya ya Taasisi ya Uongozi inamshukuru Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi huo na watafanya kazi na kuhakikisha wanafikia lengo kuu la kujenga viongozi watakaoleta maendeleo endelevu nchini.
Dkt. Tax amesema, Wanatambua umuhimu wa viongozi mahiri na watasimamia jukumu hilo katika kuhakikisha viongozi wanajengwa katikla miiko ya maadili na kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi.
''Sio kwamba viongozi hawapo....Wapo ila mambo yanabadilika kila siku lazima viongozi waende na maendeleo ya kidunia.'' Amesema Dkt. Tax.
Awali akieleza majukumu ya Taasisi hiyo Afisa Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute,) Dkt. Kadari Singo amesema, Taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuandaa na kuendesha mafunzo kwa viongozi, kuendesha majadiliano ya kisera na kufanya tafiti za kisera, kutoa ushauri wa kitalaam na kuzisaidia taasisi mbalimbali pamoja na viongozi wake katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute,) ilianzishwa Julai, 2010 kwa malengo ya kuwa na kituo cha utalaam wa juu cha kuendeleza viongozi barani Afrika kwa kuanzia nchini Tanzania, Kanda za Afrika Mashariki na hatimaye Afrika nzima.
No comments:
Post a Comment