Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kimamba Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
RAIS wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suruhu Hassan amefuta mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24119 na kufufua mashamba 49 yenye ekari 45788.3 ambayo yamefutwa hatimiliki yake wilayani kilosa Mkoa wa Morogoro na kuagiza mashamba hayo kugawiwa kwa wananchi ambao hawana mashamba ya kulima.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kimamba Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi amesema Mhe Rais Samia ametoa Ekari 1000 kwa kijiji hicho kama kifuta jasho hivyo ardhi hiyo isitumike kuwa chanzo cha migogoro ya Ardhi.
“Ardhi hii imetolewa na Mhe Rais kwa ajili ya kulima katani na sisi tutafurahi zaidi kama mtawakaribisha wawekezaji wakubwa waje kulima katani hapa ili waweze kuinua uchumi wa wanakimamba”.alisema Waziri Lukuvi.
Aidha amesema wizara ya Ardhi imetuma tume itakayoongozwa na kaimu Kamishina wa Ardhi Mkoa wa morogoro katika kuhakikisha mashamba yote yaliotolewa na Mhe Rais yanapangiwa matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Morogoro Bwana Martin Shigela amemuhakikishia Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi kuwa atawashughulikia viongozi wote wa vijiji wanaosababisha migogoro ya Ardhi katika Wilaya ya Kilosa na Mkoa kwa ujumla
Ameongeza kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya Ardhi ni viongozi wa vijiji ambao wanauza mashamba bila ya kufuata taratibu na kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima na kuutia doa Mkoa na kuufanya kuwa kitovu cha migogoro ya Ardhi.
Nae Mbunge wa Jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa katiba na sharia Mhe Palamagamba Kabudi Akizungmza na wananchi wa vijiji vya Kimamba na Ilonga amewataka wananchi kutunza Ardhi waliopatiwa na Mhe Rais kwa ajili ya kilimo.
Nao wakazi wa Wilaya ya kilosa wamemshukuru Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kuwarudishia mashamba hayo kwa ajili ya kilimo cha katani kwani wengi walikuwa wanatamani kulima katani lakini hawana maeneo ya kulima kutokana na mshamba mengi kumilikiwa na Taasisi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment