Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoshiriki katika ujenzi
wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Ruangwa kulinda
fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa
kuvitunza vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi ili mradi ukamilike kwa
wakati.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Samia
Suluhu Hassan ameridhia kutolewa kwa fedha za ujenzi huo hivyo ni lazima
zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Ametoa
kauli hiyo leo (Juni 7, 2021) wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi
wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kijiji cha
Nandagala wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.
“Rais wetu anatupenda
ndiyo maana katuletea pesa ambazo lazima tuzilinde, tukinunua vifaa vya
ujenzi kama vile, mabati, saruji, mbao na nondo lazima vyote vitumike
hapa kwenye ujenzi na kamwe tusiruhusu udokozi”
Waziri Mkuu
amesema kuwa serikali itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi na yeye
akiwa mbunge wao anawajibika kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha
Ruangwa inasonga mbele katika nyanja zote.
Pia Waziri Mkuu
ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Uongozi wa VETA na
Suma JKT kwa kusimamia kwa weledi na uaminifu ujenzi wa chuo hicho na
amewataka kuhakikisha kwamba ujenzi unakamilika kwa wakati ili mafunzo
yaanze kutolewa.
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema
chuo hicho kitajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu
shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 1.2.
Amesisitiza kuwa mafunzo ya muda mrefu katika chuo hicho yanarajiwa kuanza mwenzi Januari 2022 kwa mujibu wa mafunzo ya VETA.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema kuwa Chuo kitakuwa ni
kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wakazi wa eneo la Nandagala na
wilaya ya Ruangwa hivyo wazazi wawapeleke watoto wao wakajipatie maarifa
na ujuzi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Faraji Magama ambaye ni Mshauri Mwelekezi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Ruangwa wakati alipofugua ujenzi wa Chuo hicho katika kijiji cha Nandagala wilayani humo, Juni 7, 2021. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ruangwa katika kijiji cha Nandagala, Juni 7, 2021.



Baadhi ya viongozi na wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Ruangwa katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa, Juni 7, 2021.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment