Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa soko la Mirerani, Mkoani Manyara, Yesaya Songelael Yindi amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 407,000 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Simanjiro, Yefred Myenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, ameyasema hayo ofisini kwake mjini Babati, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Makungu amesema pia, Mahakama hiyo ya Wilaya ya Simanjiro, imemuhukumu kifungo cha kwenda jela miezi 12 au kulipa faini ya shilingi milioni moja mfanyabiashara wa mji mdogo wa Mirerani Antipas Benedict Ngelesh kwa kosa la kukaidi amri halali ya Mkurugenzi huyo ya kubomoa kibanda.
Amesema wafanyabiashara hao wamehukumiwa kwenye kesi hiyo ya jinai namba 47/2020 na Hakimu wa mahakama ya wilaya ya hiyo ya Simanjiro Nicodemo Onesmo.
Amesema kwenye hukumu hiyo mstakiwa Songelaeli amefanya kosa hilo kinyume na kifungu cha kuzuia rushwa cha 15 (1) (b) na 15 (2) ya cha sheria ya kuzuia rushwa namba 11/2007.
Amesema awali, mawakili wa TAKUKURU, Martin Makani na Evelin Makani waliwasilisha ushahidi usioacha shaka mahakamani hapo na kusababisha adhabu hizo kwa washtakiwa hao.
Amesema Mahakama hiyo iliridhika kupitia ushahidi huo na vielelezo kuwa Songelaeli ambaye ni Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mirerani alimtumia Myenzi rushwa kwa njia ya mtandao ili asivunje kibanda hicho cha kuoshea magari kilichojengwa na Ngelesh nje ya utaratibu.
Amesema Songelaeli mwenye ushawishi mkubwa kwenye eneo hilo alimtumia Myenzi fedha hizi kwa njia ya rushwa ili amshawishi kubadili amri ya kuvunja kibanda hicho cha Ngelesh ambaye naye hakukivunja ili kutekeleza agizo hilo hadi walipokamatwa na TAKUKURU na kufikishwa Mahakamani.
Amesema Mahakama iliwatia hatiani washtakiwa wote wawili kama walivyoshtakiwa huku wakili wa utetezi Shirima akiwaombea huruma washtakiwa hao kwa kutokuwa na taarifa za uhalifu huko nyuma, matatizo ya kiafya na watoto wanaowategemea huku mawakili wa TAKUKURU wakiiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.
"Ni rai yetu watumishi wa umma mkoani Manyara, kukataa rushwa kwa kutoa taarifa TAKUKURU kama alivyofanya Mkurugenzi wa Simanjiro Myenzi, ikiwa wote tutashirikiana na kuzingatia misingi ya uadilifu tuliyojiwekea katika utumishi wa umma vita dhidi ya rushwa itakuwa nyepesi na watoa rushwa nao hawatatoa watahofia sheria kuchukua mkondo wake." amesema Makungu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
No comments:
Post a Comment