Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amewahamasisha
wafanyabiashara wa Kitanzania kuendelea kufanya biashara na kwenda
kuwekeza nchini Kenya kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo
iliyopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na amewataka kuwasiliana na
Wizara iwapo kutakuwa na changamoto zozote.
Hayo ameyasema
katika Mkutano wa tano (5) baina ya Tanzania na Kenya kwa ajili ya
kujadili masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo vikwazo vya biashara
visivyokuwa vya kiushuru (NTBs) baina ya nchi hizo uliofanyika kuanzia
tarehe 26 hadi 29 Mei 2021 katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
Katika mkutano huo Waziri wa
Viwanda na Biashara Prof. Mkumbo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki
Mkutano huo ambao ulijumuisha Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu –
Uwekezaji, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda –
Zanzibar, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, wakati
ujumbe wa kenya ukiongozwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo
ya Wajasiliamali Mhe. Betty Maina aliyeambana na Balonzi wa Kenya nchini
Tanania
Aidha, Waziri amesema kuwa mkutano huo ni utekelezaji
wa maelekezo ya kuimarisha mahusiano ya biashara na nchi jirani
yaliyotolewa katika Ziara ya Kiserikali iliyofanywa nchini Kenya na,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe
4-5 Mei 2021.
Prof. Mkumbo amesema Mkutano huo wa kibiashara
baina ya nchi hizo ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya biashara
katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji. Jumla ya
masuala 64 yamejadiliwa ambapo kati ya hayo masuala 30 yametatuliwa na
mengine 34 yaliyobaki yamewekewa mkakati maalum na muda wa utekelezaji.
Miongoni
mwa masuala yaliyotatuliwa kwa upande wa Tanzania ni pamoja na
kuwezesha upitishaji wa bidhaa mpakani, hususan vinywaji baridi kama
vile juisi kutoka Tanzania kwenda Kenya, kuondolewa kwa tozo za ukaguzi
(inspection fees) zilizokuwa zinatozwa na Mamlaka za Kenya kwenye bidhaa
za Tanzania, ikiwemo unga wa ngano, zenye alama ya ubora kutoka Mamlaka
husika Tanzania, kuwezesha upitishaji wa mahindi kutoka Tanzania kwenda
Kenya na Kuondoa ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za kioo kutoka
Tanzania kwenda Kenya. Amefafanua Prof. Mkumbo.
Kwa upande wa
Kenya, masuala yaliyotatuliwa ni pamoja na kutoa upendeleo kwa bidhaa za
sementi zinazozalishwa nchini Kenya ambazo zinakidhi matakwa ya vigezo
vya uasili wa bidhaa vya na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutoa upendeleo
maalum kwa vinywaji kutoka Kenya ikiwemo juisi za nanasi (Pineapple
Juices) baada ya kukidhi vigezo vya uasili wa bidhaa vya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Masuala mengine ni pamoja na kuhakikisha
bidhaa zinazoharibika haraka kama vile maziwa zinapewa kipaumbele
zinapovuka mpaka kutoka Kenya kuingia Tanzania kwa kuzingatia taratibu
za Sheria ya Forodha na kuongeza muda (validity period) wa kibali cha
kuingiza bidhaa za mifugo kutoka siku 15 hadi siku 30. Amefafanua Prof.
Mkumbo
Pia, Prof Mkumbo amesema kabla ya Mkutano wa Mawaziri
ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu kutoka nchi hizo uliofanyika
Mei 28, 2021 jijini Arusha. Ujumbe huo wa Tanzania ulijumuisha Makatibu
Wakuu kutoka kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Biashara na
Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar,Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
(Uchukuzi), Kaimu Katibu Mkuu –Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Kaimu Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, na Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania.
Aidha,
wajumbe wa mkutano huo baina ya nchi hizo walipata fursa ya kutembelea
mpaka wa Namanga pande zote mbili na kujionea jinsi biashara na shughuli
za upitishaji wa bidhaa na huduma zinavyofanyika katika mpaka huo ikiwa
na Lengo la kuwahakikishia wafanyabiashara kuwa maagizo ya Waheshimiwa
Marais wa Tanzania na Kenya yamefanyiwa kazi kikamilifu na wanatakiwa
kufanya biashara kwa kuzingatia sharia taratibu na miongozo iliyopo
Katika
makubaliano hayo, nchi hizo zilikubaliana kuunda Timu ya Maafisa
Wanne(4), yaani Maafisa Wawili (2) kutoka kila Nchi, kwa ajili ya
kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano huu, na
kuhakikisha kuwa vikwazo vilivyotatuliwa havijitokezi tena.
Pia,
amesema kuwa nchi hizo zimekubaliana kudumisha ushirikiano baina yake
hususan katika nyanja za uchumi, biashara na uwekezaji kwa kufuata
taratibu zote zinazokubalika kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo
nchi hizo mbili ni wanachama.
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na
Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya Mhe. Betty Maina amesema
amefurahishwa na mkutano huo kwani umeweza kutekeleza maagizo ya Marais
wa nchi hizo mbili na kufanikiwa kutatua masuala 30 na ameahidi ndani ya
miezi mitatu watahakikisha changamoto zilizobaki watazimaliza na
kufanya wafanyabiashara wa hchi mbili hizo wanafanya biashara bila
vikwazo vyovyote.
Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara kati ya
nchi hizo mbili kufuata taratibu na sheria zilizopo katika biashara
baina yao ili kukuza uchumi wa nchi zao kwa kushirikiana na kutumia
bidhaa zinazozalishwa kati ya nchi hizo.
Nchi hizi mbili
zimekuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara kujadili masuala
mbalimbali yanayohusu Biashara na Uwekezaji. Mikutano hiyo imekuwa
ikiwakutanisha Wataalamu kutoka Wizara, Taasisi za Serikali wawakilishi
wa Sekta Binafsi pamoja na Wafanyabiashara. Kupitia mikutano hiyo,
masuala mbalimbali vya biashara yamekuwa yakijadiliwa na vikwazo vya
biashara vinavyojitokeza kupatiwa ufumbuzi.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo akiongoza kikao cha
majidiliano ya masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo kuondoa vikwazo
vya biashara visivyokuwa vya kiushuru baina ya nchi ya Tanzania na Kenya
katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji kwenye kikao
kilichofanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini
Arusha, 29 Mei 2021.
Waziri
wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya, Mhe.
Betty Maina na ujumbe kutoka hizo nchi mbili wakiwa majidiliano ya
masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo kuondoa vikwazo vya biashara
visivyokuwa vya kiushuru baina ya nchi ya Tanzania na Kenya katika kikoa
kilichofanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini
Arusha, 29 Mei 2021.
Waziri
wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo na Waziri
wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya, Mhe.
Betty Maina wakisaini makubaliano ya kutatua masuala mbalimbali ya
biashara katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji
kwenye kikao cha Pamoja cha nchi hizo katika ukumbi wa Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha, 29 Mei 2021.
Waziri
wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo na Waziri
wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya, Mhe.
Betty Maina wakibadilishana nyaraka zilizosainiwa makubaliano ya
kuondolewa kwa masuala 30 na mengine 34 yaliyobaki yamewekewa mkakati
maalum na muda wa utekelezaji ya kuondoa kuondoa vikwazo vya biashara
visivyokuwa vya kiushuru baina ya nchi ya Tanzania na Kenya katika
ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha, 29 Mei
2021.
Mawaziri
wa Tanzania na Kenya na ujumbe walioambatana nao wakiwa kwenye kikao
cha majidiliano ya masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo kuondoa
vikwazo vya biashara visivyokuwa vya kiushuru baina ya nchi ya Tanzania
na Kenya katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji
kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
(AICC) jijini Arusha, 29 Mei 2021.
Picha Zote na Eliud Rwechungura
No comments:
Post a Comment