WATUMISHI wa UMMA mkoa Iringa wametakiwa kuwa mfano kwa wananchi kwa kuhakikisha wanakuwa na mashamba ya kimkakati yatakayowasaidia wananchi kujifunza ikiwa ni pamoja na wao kujiinua kiuchumi .
Akizungumza kwenye kikao cha wakuu wa taasisi za UMMA za mkoa wa Iringa cha kujitambulisha kwa mkuu wa mkoa mpya Queen Sendiga,katibu tawala wa mkoa huo Happiness Seneda alisema kuwa mkoa wa Iringa umebarikiwa kuwa na ardhi ambayo inafaa kwa kilimo cha mazao yoyote yale
Seneda alisema kuwa watumishi wengi wa umma wamekuwa na hali ngumu kutokana na kutowekeza kipato chao katika ardhi jambo linalowaletea ugumu hasa pale wanapopata matatizo ya kufiwa au kufariki wao wenyewe.
Aliongeza kusema kuwa watumishi wengi wa Umma wamekuwa wakijikita katika vitendo vya anasa kama ulevi na uzinzi hali inayosababisha mishahara yao kutumika bila malengo na kuzifanya familia zao kuishi katika mazingira magumu.
“Watumishi wenzangu wa sekta za umma tunajisahau kwa sababu tunakuwa na uhakika wa kupata mishahara na malupulupu basi tumekuwa ni wanywaji pombe wa kupindukia tumekuwa wazinifu mwisho wasiku tunapata tabu pale mnapofariki maana unakuta nyumbani hakuna hata kitu cha kuanzia” alisema Seneda
Awali akizungumza mkuu wa mkoa wa Iringa Mh. Queen Sendiga alisema mkoa umejipanga kuja na kilimo mkakati kitakachowainua wananchi kiuchumi hivyo watumishi wa umma wanatakiwa kuwa mfano kwa kuwa na mashamba ya kilimo cha biashara.
Alisema ni aibu kwa mkoa wa Iringa kuonekana wananchi wake wanalia umasikini wakati mkoa umebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayozalisha mazao ya aina mbalimbali kama alizeti, nyanya, palachichi, mpunga mahindi na mengineyo.
Sendiga alisema mkakati walionao ni kuona kila kaya inakuwa na mashamba ya kulima na katika mashamba hayo eka moja ni lazima liwe shamba la kilimo maalumu cha biashara ili kuwainua wananchi wake.
‘’Niseme wazi ninachukizwa na hali ya wananchi wa mkoa wa Iringa wakati wamerikiwa ardhi yenye rutuba nyingi ya kilimo mkoa sasa umekuja na mkakati wa kuhakikisha kila kaya inakuwa nae ka moja ya kilimo maalumu cha zao la biashara na nitafuatilia hilo ukiona umelima kilimo kile cha mazoea hakikisha una eka moja ya kilimo biashara”alisema Sendiga.
Wakizungumza baadhi ya wakazi wa mkoa wa Iringa wamesema kuwa mkakati aliokuja nao mkuu wa mkoa ni mzuri na utawainua wananchi wa mkoa wa Iringa ambao wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea japo changamoto huwa katika suala la pembejeo.
No comments:
Post a Comment