HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 18, 2021

Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB kuweka historia mpya

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa Benki hiyo unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi Mei 22, 2021, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki. Kulia ni Mkurugeni wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa na kulia ni Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo.

=====  ====  ====

Benki ya CRDB inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa siku ya Jumamosi tarehe 22/05/2021 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mkutano huo unafanyika kufuatana na Sheria ya Makampuni (Companies Act) namba 212 ya mwaka 2002, ambapo kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki.
Akizungumzia katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Mount Meru Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela amesema ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki mkutano huu muhimu, Benki ya CRDB imeandaa utaratibu kwa wanahisa ambao kwa namna moja au nyingine hawatoweza kufika Arusha waweze kushiriki mkutano wa kwa njia za kidigitali. 
“Kwa kuzingatia uzoefu tulioupata kwa kufanya mkutano wa 25 kwa njia ya mtandao, wanahisa walipitisha pia azimio la mkutano wa 26 kufanyika kwa njia zote mbili kwa maana ya kuruhusu wanahisa wanaoweza kushiriki kwa kufika Arusha lakini pia kuruhusu wanahisa wanaoweza kushiriki kwa njia ya mtandao kutumia njia hiyo ambapo itakua ni historia kwa mkutano mkuu wetu kufanyika nama hii” alisema Nsekela.

Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utatanguliwa na semina maalum kwa wanahisa yake ili kukuza uelewa wa masuala mbalimbali ya fedha na uwekezaji katika masoko ya mitaji. Semina hiyo itafanyika siku ya Ijumaa tarehe 21/05/2022 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mgeni Rasmi katika semina hiyo anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Mwigulu Nchemba ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wa masuala ya fedha, sheria na uwekezaji katika masoko ya mitaji. 
Kwa mujibu wa Nsekela hii itakua ni mara ya kwanza kwa Mkutano wa Mkuu wa Wanahisa wa Benki ya CRDB kufanyika kwa njia zote mbili ambapo mkutano wa mwaka jana ulikuwa wa kwanza kwa Benki kutumia njia za kidigitali ili kukabiliana na changamoto ya COVID-19. Zaidi ya wanahisa 1400 waliweza kushiriki mkutano wa mwaka jana idadi ambayo haijawahi kufikiwa katika mikutano ya kawaida ambayo hufanyika jijini Arusha kwa miaka yote.

“Nachukua fursa hii kuwakaribisha wanahisa wote katika semina na mkutano mkuu na niwahakikishie wanahisa wote ambao watashiriki kwa njia ya mtandao kuwa tumejipanga vizuri katika kuhakikisha kila wanashiriki kama wanahisa ambao watakua AICC na tumeweka maelezo katika tovuti yetu ya Benki (www.crdbbank.co.tz) ya jinsi gani wanaweza kushiriki hatua kwa hatua” aliongeza Nsekela.
Pamoja na mambo mengine yatakayojadiliwa katika mkutano mkuu huo ikiwemo maboresho ya katiba ya kampuni, shauku kubwa kwa wanahisa ni kufahamu juu ya pendekezo la gawio kwa wanahisa kwa mwaka uliopita ukizingatia kuwa Benki ya CRDB imeendelea kupata matokeo mazuri sokoni ambapo katika hesabu za mwaka wa fedha ulioisha Benki iliweza kupata faida kabla ya kodi ya Shilingi Bilioni 236 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kutoka Shilingi Bilioni 175 iliyopatikana mwaka 2019. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad