HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 4, 2021

MAENDELEO YA VIWANDA YAENDANE NA HIFADHI YA MAZINGIRA - WAZIRI JAFO

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Mashariki kusini Bw. Hamad Taimur (hayupo pichani) kuhusu Kiwanda cha Saruji cha Diamond ambacho kimekithiri kwa uchafuzi wa mazingira. Waziri Jafo amefanya ziara hiyo leo Mei 4, 2021. Watatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkurunga Bw. Filberto Sanga.

Na Lulu Mussa. Dar es Salaam
SERIKALI imesema kamwe haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaolenga kuwekeza katika sekta ya viwanda bali maendeleo ya viwanda ni lazima yaende sambamba na hifadhi ya Mazingira.

Rai hii imetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo katika ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira katika Kiwanda cha saruji cha Diamond na Kiwanda cha kutengeneza nondo cha Lodhia Steel Industry vilivyopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Katika ziara ya kukagua kiwanda cha Saruji Waziri Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa Kiwanda hicho kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa mazingira kutokana na kukithiri kwa vumbi linalosababishwa na shughuli za uzalishaji wa saruji kiwandani hapo.

“Nimekuja hapa kufuatia malalamiko mengi ya wananchi na wakazi wa maeneo haya wamiliki wa kiwanda hiki wamezima mitambo yote wakijua nakuja, wamekimbia hivyo NEMC chukeni hatua mara moja, watozwe faini na nipate taarifa mapema Ofisini” Jafo alisisitiza.

Hata hivyo, Waziri Jafo ameridhishwa na uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika Kiwanda cha Lodhia Steels Industry na kuwataka wawekezaji wengine kwenye sekta ya viwanda kuiga mfano wa kiwanda hicho kwa kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinafanyika bila kuharibu mazingira na kuhatarisha afya za binadamu na viumbe hai.

“Katika Viwanda vyote vinavyofanya shughuli ya uzalishaji wa nondo hapa nchini, kiwanda hiki ni mfano wa kuigwa katika kuhifadhi na kutunza mazingira, pia kimetoa ajira kwa watanzania wapato 700 na kuzalisha tani 200 za nondo kila siku zenye ukubwa wa milimita 8 - 40 ambazo zinatumika katika miradi ya kimkakati hapa nchini kama ujenzi wa Reli ya Kisasa, Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere pia daraja za Tanzanite” Jafo alisisitiza.

Jafo ametoa onyo kwa waharibifu wa miundombinu ya nchi kwa kigezo cha kuuza chuma chakavu na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wabadhirifu wa mali ya umma.

“Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara, baadhi ya watu wanaokoteza mitaani chuma chakavu, tusipokuwa wakali tutatengeneza miundombinu na kuharibu miundombinu pia, lazima tulinde miundombinu ya Nchi” aliongezea Waziri Jafo.

Mkurugenzi wa Lodhia Steel Bw. Saileth Pandit ameiomba Serikali kufanya mabadiliko ya Sera na mikataba ya kimataifa inayozuia uingizwaji wa malighafi ya chuma chakabu kutoka nje ya nchi ili kuwezesha viwanda kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za chuma hapa Nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad