HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 20, 2021

TAKUKURU MWANZA YAMTIA MBARONI ALIYEKUWA MHASIBU WA BANDARI KIGOMA

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza mnamo tarehe 19/04/2021 imemkamata aliyekuwa Mhasibu wa Mamlaka ya Bandari Kigoma Bw. Madaraka Robert Madaraka ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya Rushwa, Uhujumu Uchumi na Ukwepaji Kodi wa kiasi cha Sh. 153,543,550/=.


Bwana Madaraka Robert Madaraka ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wa waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority-TPA) Mkoa wa Kigoma, amekamatwa akiwa mafichoni katika eneo la Nyasaka Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.

Mtuhumiwa huyu amekuwa akitafutwa na TAKUKURU tangu mwezi Agosti, 2020 ili aweze kuunganishwa katika tuhuma hii na wenzake watano (5) ambao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma tangu tarehe 31, Agosti 2020.

Washitakiwa hao ni:-
Rodrick Ndeonasia Uiso-Mkurugenzi wa Kampuni ya Saxon Building Contractors Limited
Ajuaye Kheri Msese -Aliyekuwa Meneja wa Bandari Kigoma
Herman Ndiboto Shimbe-Aliyekuwa Afisa Uhasibu TPA Kigoma
Jesse Godwin Mpenzile –Aliyekuwa Mhandisi Mkazi TPA Kigoma
Lusubilo Anosisye Mwakyusa –Aliyekuwa Afisa Rasilimali watu TPA Kigoma
Aidha, ikumbukwe kwamba wakati watuhumiwa hao wanafikishwa Mahakamani tarehe 31/08/2020, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alitoa taarifa kwa umma juu ya kutafutwa kwa Bwana Madaraka Robert Madaraka.

Pamoja na kumkamata Bw. Madaraka Robert Madaraka aliyekuwa anatafutwa na TAKUKURU, napenda kutumia hadhira hii kuuhabarisha umma juu ya utendaji kazi wa ofisi yangu kwa kipindi cha Januari – Machi 2021.

Katika kipindi cha mwezi Januari - Machi, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kuokoa fedha zaidi ya Shilingi millioni 87 ambazo zilirejeshwa katika operesheni za kufuatilia fedha za umma zilizokuwa zimechepushwa au kufanyiwa ubadhirifu, kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007. Vilevile katika kipindi husika, tumefungua kesi mpya 8 Mahakamani.

Kati ya fedha hizo zilizookolewa:
Kiasi cha Sh. 14,048,358/= zimewekwa kwenye akaunti maalum iliyopo Benki kuu
Sh. 73,168,275/= zimerejeshwa kwa wahusika mara baada ya kuokolewa,
Sh.38,006,275 zimerejeshwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri,
Sh. 4,345,000/= zimekabidhiwa kwa Vyama vya Ushirika,
Sh.18,549,200/= wamerejeshewa wananchi waliodhulumiwa kupitia mikopo umiza, na
Sh. 12,267,800/= wamekabidhiwa watumishi wa Sekta Binafsi ambao waliofanyakazi bila kupata stahiki zao kutoka kwa waajiri wao.

Katika kipindi cha Januari-Machi, 2021 TAKUKURU mkoa wa Mwanza imekamilisha uchunguzi wa majalada 12, imefungua kesi mpya 8 na kupokea taarifa 280 za malalamiko ya vitendo vya rushwa.

Aidha, Serikali za Mitaa (Wenyeviti na watendaji wa vijiji, mitaa, vitongoji na kata) zinaongoza kwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ambapo ina malalamiko 51 kati ya taarifa 280 zilizopokelewa ikifuatiwa na idara ya Ardhi malalamiko 35, Elimu 35,Taasisi binafsi malalamiko 33, Taasisi za mikopo 27, Taasisi za fedha 18, Biashara 12, Vyama vya ushirka 10, Uvuvi 8, Mahakama 6, Polisi 5,Taasisi za dini 4,mifuko ya hifadhi ya jamii 4, Ujenzi 3, maji 3, Afya 3, BIMA 3, TRA 2,Mifugo 2, Madini 2,Siasa 2, Marine 2,michezo 1,Uhamiaji 1,TANESCO 1, Habari 1, Vyama vya wafanyakazi 1,TPA 1,Sheria 1, TBA 1, ,mazingira 1 na misitu 1.

Kwa upande wa ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo TAKUKURU mkoa wa Mwanza katika kipindi cha mwezi Januari-Machi, 2021, imefanya ukaguzi wa miradi 14 yenye thamani ya Sh.11,408,633,077.32/=.

Kati ya miradi hiyo 14 iliyokaguliwa, miradi 7 inahusu ufuatiliaji wa fedha za maendeleo ya jamii awamu ya tatu TASAF yenye thamani ya

Sh. 2,232,960,760/=, miradi 5 ya elimu yenye thamani ya
Sh. 742,153,279.11/= na miradi 2 ya ujenzi yenye thamani ya
Sh.8, 433,519,038.21 /=. Aidha, kati ya miradi hiyo 14 iliyokaguliwa miradi 8 imekamilika na miradi 6 inaendelea na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Pamoja na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU mkoa wa Mwanza kupitia dawati lake la uzuiaji rushwa imefanya vikao vya warsha 4 na uchambuzi wa mfumo kuhusu utoaji wa vibali vya ujenzi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza, kwa lengo la kutathmini mfumo wa utoaji wa vibali vya ujenzi unaofanywa na Halmashauri kote nchini.

Aidha wakati wa uchambuzi wa mfumo kuhusu utoaji wa vibali vya ujenzi TAKUKURU imebaini mapungufu mbalimbali kama ifuatavyo:-

Halmashauri kutofuata muongozo wa serikali wa utoaji wa vibali vya ujenzi
Taratibu za kupata kibali cha ujenzi kutokufahamika kwa baadhi ya wananchi
Halmashauri kutotenga bajeti ya wataalam ya kufanya kazi ya uidhinishaji wa vibali vya ujenzi
Halmashauri kutofanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye majengo/ ujenzi unaondelea
Watendaji wa kata kutotambua wajibu wao wa kufanya ukaguzi wa vibali vya ujenzi katika maeneo yao.

Hivyo kutokana na changamoto hizo TAKUKURU imekaa na watendaji wa baadhi ya Halmashauri wanaohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi na kuwakumbusha wajibu wao juu ya umuhimu wa kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali.

Kwa upande wa elimu kwa umma katika kipindi cha Januari-Machi, 2021, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imeweza kuzuia vitendo vya rushwa kwa kutoa elimu na kuyafikia makundi mbalimbali kwa kufanya semina 37, mikutano ya hadhara 57 ,vipindi 5 vya redio, Uandishi wa habari na makala 9, taarifa kwa vyombo vya habari 4, maonesho 13 na kuimarisha klabu 83 za wapinga rushwa kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo.

TAKUKURU INAYOTEMBEA:
Hapa eleza juu ya uwepo wa utaratibu wa TAKUKURU inayotembea. Nini mmebaini na nini mmechukua hatua.

MIKAKATI YA APRILI – JUNI 2021

TAKUKURU Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha April-Juni 2021 itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa mujibu wa sheria kwa kuchunguza makosa ya rushwa na kufuatilia fedha za Serikali na wafadhili zinazofanyiwa ubadhirifu.


Wito kwa wananchi;
Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza na watumishi wote katika Taasisi za umma na Taasisi binafsi, kila mmoja kwa nafasi yake awajibike kwa kuhakikisha mnaepuka vitendo vya rushwa, mnazingatia sheria kanuni na taratibu za kazi, na kutoa huduma bora kwa wananchi pasi kuwa na vikwazo vya rushwa.

Aidha ninawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili tuweze kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.

PALIPO NA RUSHWA HAKUNA HAKI
“Kwa taarifa za vitendo vya rushwa fika ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nawe au piga simu ya dharura namba 113 au tuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au Piga *113# fuata maelekezo” Huduma hii ni ya BURE.

IMETOLEWA NA:
FRANK MKILANYA- 0738 150 162
MKUU WA TAKUKURU (M) MWANZA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad