SHINDANO maalumu la 'The Capital Markets, Universities and Higher Learning Institutions Challenge' kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu za Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar lililoendeshwa kwa njia ya Teknolojia ya Mawasiliano na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana limefika tamati na jumla ya washindi 80 sawa na asilimia 0.4 ya washiriki 21338 wamepatikana na kupatiwa zawadi zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA Nicodemus Mkama alisema kuwa Mamlaka hiyo iliendesha shindano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu kwa malengo ya kujenga uelewa na weledi wa masoko ya mitaji na uwekezaji nchini.
"Shindano hili lilifunguliwa Agosti 4,2020 na kufungwa Novemba 30, 2020 na liligawanyika katika makundi mawili ambalo kundi la kwanza lilikuwa ni la kujibu maswali 100 yaliyolenga kujenge uwezo kwa washiriki kuhusiana na masuala ya masoko ya mitaji na uwekezaji, na kundi la pili lilikuwa ni la kuandika Insha ya kueleza fursa na faida zinazopatikana katika uwekezaji wa masoko ya mitaji kwa mifano." Amesema.
Mkama amesema, katika mashindano hayo washindi ni wale waliopata alama za juu kuzidi washiriki wengine na hafla hiyo ni muendelezo ya kujenga uelewa zaidi kuhusiana na masuala ya masoko ya mitaji na uwekezaji, sekta ambayo inazidi kuendelea zaidi kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
"Ushiriki wa wanafunzi umezidi kuongezeka zaidi kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambapo tunatumia simu za mkononi, Internet na barua pepe katika kuwafikia washiriki na tunaona wanafunzi hapa wametoka katika vyuo mbalimbali ikiwemo Mzumbe- Morogoro, Dar es Salaam, UDOM,St.Joseph, St.Augustine na Zanzibar." Amesema.
Amesema shindano hilo ni la kwanza kufanyika barani Afrika kwa kutumia Teknolojia ya Mawasiliano na limekuwa kivutio kwa wasimamizi wengi wa masoko ya mitaji barani humo na wengi wametoa hitaji la kutaka kujifunza na kuliendesha katika nchi zao.
Katika shindano hilo mshindi wa kwanza kwa kila shindano amezawadiwa fedha za kitanzania shilingi milioni moja na laki nane, mshindi wa pili milioni moja na laki nne, mshindi wa tatu shilingi laki nane, washindi wa tano hadi 20 shilingi laki mbili na washindi walioingia katika fainali wamepatiwa vyeti vya utambuzi pamoja na T-Shirt.
''Washindi watatu waliopata alama za juu katika makundi yote watagharamiwa ziara ya kwenda kujifunza na kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inagharamiwa na Mamlaka ya Masoko ya mitaji na Dhamana, Mamlaka hii uwekezaji wa Trilioni 29 fedha za kitanzania ambapo trilioni 15 ni uwekezaji katika hisa, Trilioni 11 ni hati fungani (serikali na kampuni,) na Bilioni 500 ni uwekezaji wa mifuko ya pamoja hii inathibitisha umuhimu wa Mamlaka hii katika sekta ya fedha na uchumi.'' Amesema.
Shindano hilo lililoanza na washiriki 2000 limefikia kiwango cha kuwafikia washiriki 20,000 zaidi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar huku matunda ya mashindano hayo yakionekana kwa baadhi ya washiriki kuwekeza katika masoko ya mitaji na mifuko ya pamoja.
No comments:
Post a Comment