Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesema Ofisi yake inaandaa Kampeni kubwa ya Mazingira itakayoenda sambamba na mashindano katika ngazi mbalimbali ikihusisha upandaji miti, utunzaji na usafi wa mazingira kwa ujumla wake.
Akizungumza wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya Ofisi yake pamoja na waandishi wa habari kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, Mhe. Jafo amesema kampeni hiyo kubwa na ya aina yake itazinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani tarehe 5 Juni 2021 kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa kielelezo katika utunzaji wa mazingira.
“Kampeni hii kubwa itahusisha Mikoa yote 26 na itahusu usafi na Utunzaji wa Mazingira kwa ujumla wake ambapo tuzo na zawadi zitatolewa kwa washindi katika ngazi mbalimbali mara baada ya tathmini kufanyika na zawadi zitatolewa wakati wa Siku ya Mazingira Duniani Juni 5 mwaka 2021” Mhe. Jafo alisisitiza.
Kampeni hii pia itashindanisha Majiji, Manispaa, Halmashauri za Miji na Majiji, Kata na Vijiji. Katika nyanja za elimu na Afya, Vyuo, Shule za Sekondari, Shule za Msingi Hospitali, Zahanati na Vituo vya afya pia zitashindanishwa.
“Tunafahamu changamoto kubwa za usafiri katika mashule yetu na taasisi za elimu ya juu, zawadi kama Magari, Pikipiki, Vifaa vya kufundishia na kompyuta zitatolewa, pia vifaa tiba katika sekta ya afya ikiwemo vitanda katika hospitali zitakazoibuka vinara zitatolewa” Jafo alisisitiza.
Makundi mengine yatakayoshindanishwa ni pamoja na Viwanda, Migodi, Hifadhi za Taifa, Madampo, Viwanja vya Ndege, Stendi za Mabasi, Masoko, Hoteli za nyota (1-5) na Waandishi wa Habari za Mazingira.
“Nataka kutoa rai kwa waandishi wa Habari wa magazeti, televisheni, bloggers na mitandaoni kushiriki katika kampeni hii na mashindano haya tuzo na zawadi zitatolewa kwenu” alisisitiza Mhe. Waziri
Aidha, ameiasa jamii na watanzania kwa ujumla kupanda miti rafiki kwa mazingira hususan ile ya matunda kulingana na jiografia ya maeneo yao kwa lengo la kuboresha na kuimarisha afya zao.
Katika kampeni hii kubwa na ya kipekee jumla ya washindi 152 kutoka makundi mbalimbali watapatikana na kupatiwa zawadi ikiwa ni pamoja na kupata fursa za kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga za Wanyama hapa nchini.
No comments:
Post a Comment