HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 12, 2021

TCRA YATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTOAJI WA ELIMU KWA UMMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akimsikiliza kwa makini Waziri wake Dkt. Faustine Ndugulile akitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ofisi ya Zanzibar alipotembelea Mamlaka hiyo katika ziara yake Zanzibar akiambatana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Rahma Ali Mhe. Rahma, Makatibu Wakuu wa Wizara yake na wa Zanzibar Amour Bakari pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hizo.



Na Faraja Mpina - WMTH, Zanzibar

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu matumizi ya mtandao ‘digital literacy’ kwa kuwa mpaka sasa kiwango cha kuelimisha umma kinachotolewa na Mamlaka hiyo hakitoshelezi.


Hayo aliyazungumza Dkt. Ndugulile alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo Zanzibar tarehe 11.03.2021 akiambatana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali, Makatibu Wakuu wa Wizara yake Dkt. Zainab Chaula na wa Zanzibar Amour Bakari pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hizo.


“TCRA bado sijaridhishwa na kiwango cha elimu ya matumizi ya mtandao mnayoitoa kwa umma na katika utoaji wa elimu kwa umma mkumbuke kuelimisha jamii kuhusu wajibu na haki zao ili wanapopata shida mitandaoni wajue wapite katika njia zipi”, Dkt. Ndugulile


Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa maelekezo kwa TCRA kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa vifaa vya kielektroniki vinavyouzwa na wafanyabiashara ili kuthibitisha ubora na uhalali wa vifaa hivyo ikiwezekana viwekewe alama kuwa vimekaguliwa ili kuhakikisha usalama wa vifaa hivyo kwa matumizi ya wananchi.


Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ameielekeza TCRA kuhakikisha Shirika la Posta Tanzania linafanya kazi yake ya kusafirisha vipeto na vifurushi kwa kufuata sheria ya EPOCA inayosema kuanzia uzito wa 0 hadi 0.5 gms haruhusiwi msafirishaji yeyote kusafirisha isipokuwa Shirika hilo na kuitaka TCRA kusimamia vema suala hilo.


Hata hivyo, Dkt. Ndugulile ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule ya Sekondari ya wasichani ya Utaani iliyopo Wete Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na walimu wa shule hiyo, vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta 10, printa, projekta pamoja na kuunganisha huduma ya mtandao katika shule hiyo toka mwaka 2016 na mpaka sasa bado vipo na vinaendelea kutumika.


Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Rahma Ali ameitaka TCRA waendelee na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA huku wakijikita zaidi kwenye matumizi ya simu za mkononi. 


Kwa upande wa Mkuu wa TCRA wa ofisi ya Zanzibar Esuvatie Masinga amesema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kujipanga vizuri katika utoaji wa elimu kwa umma na wiki hii tayari wameshatoa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA kwa masheha 120 kwa Unguja na Pemba.


Kabla ya kutembelea TCRA Mawaziri hao wa pande mbili za muungano walikuwa na kikao cha pamoja kilichowashirikisha Makatibu Wakuu na wakuu wa taasisi za mawasiliano ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia hoja mbalimbali za mashirikiano katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa kuzipatia suluhisho changamoto na kuzibeba zile zinazohitaji ufuatiliaji kutoa Mamlaka nyingine ili kuendelea kuimarisha mashirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Sekta ya mawasiliano.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad