MKUU wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga amepiga marufuku watumishi wa idara ya Madini kwenda kusimamia na kukusanya mrabaha na kodi zote za serikali katika mgodi wa Bulumbaka Gasuma na badala yake mgodi huo utasimamiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU)
Marufuku hiyo ya DC Kiswaga ameitangaza mbele ya hadhara ya wachimbaji wadogo mgodini hapo, juzi.
Kiswaga anadai watumishi hao wamepewa kazi hizo kinyemela na Kaimu Afisa wa Madini Mkoa wa Simiyu, Injinia Joseph Kumburu.
"Alikuwa naye mtu huyu Kahama (Shinyanga) huko katika Mgodi unaitwa Wime.
Amemleta akusanye mapato hapa, eti ni kwa nini hiyo? Na huyo mtu ninayemsema amepewa kazi kisheria kusimamia Dutwa Two. Pale haitoshi amemleta hapa (Bulumbaka) kinyemela", alidai DC Kiswaga na kuongeza:
"Kwa mujibu wa sheria alitakiwa kama anataka kumleta mtu yeyote hapa, ashirikiane na maafisa wa kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Afisa Usalama wa Wilaya, Afisa wa Takukuru na Afisa OCD. Ndiyo angeshauriana nao.
Lakini hata kwa akili ya kawaida tu, hivi kweli Mhasibu atoke Kahama! Yaani Simiyu yote hii haina....Bariadi yote hii haina mhasibu, Bulumbaka hii hakuna mpaka atoke Kahama rafiki yake?"
Alisema mgodi huo siyo mali ya familia, hivyo alimuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bariadi (OCD) kuwakamata watu hao, punde watakapoonekana mgodini hapo wakikusanya mapato ya Serikali.
Alisema wawili hao ni mafufuku kukanyaga mgodini hapo.
"OCD, OCD hao watu wakionekana hapa kamata weka ndani," alisema DC Kiswaga na kushangiliwa na wachimbaji hao wadogo.
Jitihada za kuwapata watu hao ili wazungumzie madai hayo ya DC Kiswaga, bado zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ya Bariadi alitangaza hadharani kuwa Mgodi huo wa Bulumbaka anautambua kuwa ni eneo la rush.
Akizungumza suala hilo, Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Joseph Kumbaru alisema kwa Hana cha kuzungumza kwa sababu hakuwa na taarifa za Mkuu huyo wa Wilaya kwenda katika mgodi huo.
"Kwa Sasa siwezi kusema chochote kuhusu suala hilo, binafsi sina taarifa ya huyo Mkuu wa Mkoa, hivyo naomba unipe muda tutazungumza wakati Mwingine,"alisema Mhandisi Kumburu.
No comments:
Post a Comment