JOYCE KALINGA: MSHUMAA ULIOGOMA KUZIMIKA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 15, 2021

JOYCE KALINGA: MSHUMAA ULIOGOMA KUZIMIKA


Na Mwandishi wetu.

 “Katika kijiji cha Mninga,mkoani Iringa, watu wengi waliamini kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi,akaongoza taasisi yenye watumishi wengi kwasababu hata nilivyofika katika maeneo haya,na namna  nilivyo pokelewa haikua rahisi,wananchi wa kawaida walinishagaa kwa lugha ya kejeli na  maeneo yao  kwamba inawezekanaje mwanamke akaongoza watoto wao na kuwa mkuu wa shule,waliona ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa ila niliyashinda maneno na Imani zao potofu,  kutokana na utendaji wangu wa kazi”

Alizaliwa katika kijiji kidogo cha Ifwagi, mkoani Iringa,na kupambana, hadi kufikia ngazi ya kuwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari  Mkalala, iliyopo katika kata ya Mninga, mkoani humo.

Kutana na mwanamama Joyce Kalinga, ambae ndoto zake za kuja kumkomboa mtoto wa kike kwenye elimu, hazikukatishwa tamaa na mila potofu kutoka katika kijiji cha Ifwagi.

“Nilianzisha mwenyewe shule ya sekondari Mkalala, sikukuta mwalimu wala mwanafunzi ila nilikuta majengo na samani za kukalia wanafunzi na samani za walimu, niliweza kuanza mwenyewe kwa kusajili wanafunzi nyumba kwa nyumba kama mwalimu na pia kama mkuu wa shule, niliweza kupambana mpaka hapo serikali ilivyo ajiri walimu miezi tisa baadae”, anasimulia Joyce Kalinga.

Mwalimu Joyce Kalinga, aliweza kuanzisha kidato cha kwanza shuleni hapo, mwaka 2008, na kuweza kuwafundisha wanafunzi hao masomo yote pekee yake, bila usaidizi wa mtu yeyote.

Anasema aliweza kuwasaidia na kuwapa muelekeo ili waweze kusoma, mpaka hapo serikali ilivyo  peleka walimu katika kijiji hicho. 

 Hadi sasa shule hiyo ina walimu 17, chini ya uongozi wake wa miaka 12, ambapo wanafundisha masomo mbali mbali kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.

“Nafurahi kuwa kila mwaka, shule yangu inapanda,katika kupeleka watoto kidato cha tano hasa katika mchepuo wa masomo ya sayansi, na nimekuwa nikihamasisha watoto wa kike wachukue mchepuo wa sayansi kulingana na kizazi tulicho nacho sasa, na nimekuwa nikihamasisha sana watoto wa kike wapende kusoma, kwasababu mwanamke, ukombozi wake ni elimu. Ukipata elimu kama mwanamke, unauwezo wa kutatua changamoto mbali mbali kwasababu ile elimu uliyo ipata itaweza kumsaidia mtoto, kutatua changamoto katika jamiii, changamoto katika familia, na taifa kwa ujumla”

Ni dhahiri kuwa Mwalimu Joyce Kalinga amekuwa karibu sana na wanafunzi wake wa kike, kutokana na changamoto wanazo zipitia kijijini hapo, ikiwemo mila potofu kwamba mtoto wa kike hawezi kupata elimu bali kubaki nyumbani akisaidia kazi mbalimbai na kusubiri kuolewa.

“Nimekuwa nikisimama mimi mwenyewe, kama mmoja wa mfano, kwamba, wananfunzi wangu, waniangalie mimi, ambae nilisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne katika shule ya Mdabulo sekondari kijijini Ifwagi, na kufaulu kwenda shule ya sekondari Kilakala, mkoani Morogoro kumalizia kidato cha tano na cha sita, na kwenda kusomea ualimu katika chuo cha ualimu mkoani Morogoro. Na niliajiriwa kama mwalimu wa kawaida hadi kuteuliwa kuwa mkuu wa shule, licha ya vita vikali nilivyo kumbana navyo, nilijua nipo msituni na lazima niibuke kuwa shujaa”.

Akitolea mfano wa Makamu wa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, mwalimu Kalinga amekuwa akiendelea kuwapa hamasa  na kuamini kuwa wanafunzi wake wa kike nao watakuja kuwa viongozi mbalimbali nchini hapo baadae, ili nawo wajitambue kuwa wao ni wakina nani, na wanahitaji kupata elimu, Ili iwasaidie kufanya nini.

Katika mikutano ya walimu na wazazi, mwalimu Joyce Kalinga, amekuwa akiwaelimisha wazazi kuhusu mahitaji maalumu ya mtoto wa kike, kuwa yanahitajika kutatuliwa na kwamba wanahitaji kupewa msaada zaidi na wazazi, ili waweze kuendelea mbele, ambapo mzazi anaposhindwa kumtatulia changamoto mtoto wa kike kama zana za kila mwezi, Mwalimu Joyce huhakikisha kuwa zinapatikana kwa uraisi shuleni hapo, ili watoto wa kike wasikose masomo yao.

Katika maadhimisho ya wiki ya mwanamke duniani, yaliyo anadaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake (UN Women) pamoja na kampuni ya chai Unilever, yaliyo fanyika katika kijiji cha Mninga, kata ya Mninga, mkoani Iringa, yalitambua michango ya wanawake mbalimbali akiwemo mwanamama mwalimu Joyce Kalinga.

Mgeni rasmi ya maadhimisho hayo alikua Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri David William, ambapo aliwapongeza wanawake katika jitihada za kupambana na umasikini kwa kupiga hatua na kuwania nasafi za uongozi  kijijini hapo kwa kujiamini kuwa wanaweza.

“Nawapongeza wanawake kwa uthubutu mlio uonyesha katika kupiga vita mila potofu, na kuwapeleka watoto wa kike mashuleni ili na wao wapate elimu, kwakuwa serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Joseph Pombe Magufuli ameweza kutoa fursa kwa watanzania wote ya elimu bure, na wanawake mmeweza kuchangamkia fursa hiyo ya kuwapeleka watoto wenu wa kike mashuleni, ili na wao wapate elimu”.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jamhuri Davidi alisema kuwa amefurahishwa na wanawake  wengi walio pita kwenye uchaguzi mkuu uliopita, akiongeza kuwa wanawake wengi wamepata nafasi za uongozi kutokana na jitihada zao za utendaji wa kazi.

Joyce Kalinga ambae ametoka katika familia masikini, kutoka kijiji kidogo cha Ifwagi, kata ya Ifwagi, tarafa ya Ifwagi  mkoani Iringa, alichaguliwa kidato cha kwanza, katika shule ya Tunduru sekondari mkoani Ruvuma, ila kutokana na changamoto za hali ya hewa, mkoani humo, Mwalimu Joyce Kalinga alianza kuumwa mara kwa mara akarudi kijijini hapo na kumpumzika kwaajili ya matibabu nyumbani kwa mda wa miaka minne, alivyo pona, aliomba kurudishwa shule ili aweze kutimiza ndoto zake. Akabahatika  kupata nasafi katika shule ya Mdabulo sekondari, wilayani Mufindi, mkoani Iringa, ambapo alianza tena masomo ya kidato cha kwanza upya, wakati wenzake alio soma nao, wapo kidato cha tano.

“Safari yangu ya kuwa mwalimu haikuwa rahisi, kwasababu nilivyochaguliwa kwenda chuoni, sababu ya kukosa karo, haikunikatisha tamaa, kwahiyo mimi sikwenda nyumbani wakati wa likizo kama wenzangu, nilibaki chuoni,na kufanya kazi mbali mbali za mikono kama vile kusafisha mazingira chuoni hapo, kufyeka nyasi, kusafisha vyombo jikoni, na kuhudumia wageni  kutoka baraza la mitihani walio kuwa wanakuja kufanya kazi maalum, ili niweze kupata ada na fedha za matumizi mbali mbali binafsi”.

Amewasihi watoto wa kike pamoja na wanawake kwa ujumla, kuwa wasikate tamaa bila kutimiza ndoto zao.

Hafla hiyo chini ya shirika ya Umoja wa mataifa linalo shughulikia maswala ya wanawake (UN WOMEN), kampuni ya chai ya Unilever pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mufindi, yaliyo beba kauli mbiu isemavyo “Wanawake katika uongozi:chachu kufikia dunia yenye usawa”, iliambatana na upimaji wa afya bure pamoja na uchangiaji wa damu salama.

Hadi sasa mwanamama Joyce Kalinga amekuwa mwanamke wa kuigwa kijijini Mninga, akiwa mstari wa mbele katika kupinga mila potofu kuwa mtoto wa kike anafaa kukaa nyumbani na kusubiri kuolewa.

Katika historia  fupi ya maisha yake, amepambana na vita vikali na wanaume ambao, mwanzoni wengi wao hawakukubaliana nae, na kutaka kumuondoa kabisa kijijini hapo, kwa msemo kuwa anawaharibia mabinti zao, ila miaka 12 baadaye, wanaume wengi wameonekana kumpongeza kwa jitihada za kuhakikisha kuwa watoto wao wa kike wanashinda mashuleni, na kuepuka vishawishi pamoja na mimba za utotoni katika umri mdogo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad