Meneja Mwanadamizi wa Huduma Mbadala Benki ya CRDB, Mangire Kibanda (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya kuhamisha fedha kwa wateja wanaobashiri kati ya akaunti ya benki ya CRDB na akaunti ya mtandao ya m-bet (m-bet wallet), iliyofanyika leo kwenye hoteli ya Coral Beach iliyopo Masaki, Dar es Salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Allen Mushi (kulia) pamoja na Mejena wa Huduma ya SimBanking ya Benki ya CRDB, Emmanuel Moshi.
=======
Benki ya CRDB na kampuni ya kubashiri ya M-Bet zimezindua huduma ya kuhamisha fedha kwa wateja wanaobashiri kati ya akaunti ya benki na akaunti ya mtandao ya m-bet (m-bet wallet).
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Coral Beach iliyopo Masaki, Dar es Salaam, Meneja Mwanadamizi wa Huduma Mbadala Benki ya CRDB, Mangire Kibanda amesema huduma hiyo ambayo inapatikana katika mfumo wa SimBanking inalenga kuwapa urahisi wadau wa kubashiri kuhamisha fedha kwa ajili ya shughuli zao.
Kibanda alisema kupata huduma hiyo mteja atatakiwa kuwa amesajiliwa na huduma ya SimBanking ambayo inapatikana kupitia namba *150*03# au kwa kupitia SimBanking App.
“Mteja ataingia katika menu ya SimBanking, atachagua malipo, ataingiza kumbukumbu namba ya malipo kutoka m-bet na kisha kuhamisha fedha anazohitaji kwa ajili ya kubashili,” alielezea Kibanda huku akianisha kuwa huduma hiyo inatolewa bure bila makato yoyote kwa wateja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Allen Mushi alisema uzinduzi wa huduma hiyo unaendana na maono ya kampuni hiyo ya kuhakikisha huduma kwa wateja zinapatikana kidijitali na kunakuwa na usalama kwenye fedha za wateja.
“Tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza ya kubashiri nchini kuanzisha ubia na na Benki katika kuwawezesha wateja kuhamisha fedha kidijitali kati ya wallet zao na akaunti ya benki, hii ni habari njema kwa wapenzi wote wa kubashiri nchini kwani pia inamaanisha usalama zaidi wa fedha za wateja,” alisema Mushi.
Akielezea faida za huduma hiyo, Mushi alisema kupitia huduma hiyo wadau wa kubashiri sasa watakuwa na uwezo wa kufuatilia miamala yao, hivyo kuwajengea uwezo wa kupata taarifa za kiasi gani wamewekeza katika kubashiri na faida ambazo wanapata.
“Kupitia huduma hii mteja anaweza kutuma fedha kwenda kwenye wallet ya M-Bet lakini vilevile akishinda anaweza kuhamisha fedha zake kutoka katika wallet kwenda katika akaunti ya Benki ya CRDB ambapo anaweza kutumia kufanya manunuzi kupitia SimBanking au TemboCard yake,” aliongezea Mushi.
Akihitimisha mkutano huo, Meneja Mwanadamizi wa Huduma Mbadala Benki ya CRDB, Mangire Kibanda aliwataka wadau wa kubashiri kupitia M-Bet ambao bado hawana akaunti ya Benki ya CRDB kufungua akaunti kupitia SimBanking App kwani zoezi hilo sasa limerahisishwa.
“Mteja anachotakiwa kufanya ni kupakua rununu “application” ya SimBanking katika Play Store kwa wenye simu za Android au App Store kwa wenye simu za iOs. Itakuuliza kama una akaunti au bado, utachagua kufungua akaunti na kisha kufungua akaunti kwa kitambulisho chako cha NIDA na alama za vidole. Haijawahi kuwa rahisi hivi,” alihitimisha Kibanda.
No comments:
Post a Comment