SOMO LA HISTORIA YA TANZANIA KUANZA KUFUNDISHWA JULAI MWAKA HUU, 'TUNAMALIZIA KUANDIKA VITABU' - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 12, 2021

SOMO LA HISTORIA YA TANZANIA KUANZA KUFUNDISHWA JULAI MWAKA HUU, 'TUNAMALIZIA KUANDIKA VITABU'

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma, kulia kwake ni Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilipo. 
 
Charles James, Michuzi TV 
 
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amesema somo la Historia ya Tanzania litaanza kufundishwa Julai mwaka huu baada ya michakato ya kuandika vitabu na kuvichapisha kukamilika. 
 
Waziri Ndalichako amesema walipokea maelekezo ya Rais Magufuli aliyoyatoa Desemba 9, 2020 ya kutaka somo hilo kuanza kufundishwa ambapo wao kama wizara walianza mchakato wa kuandaa mihutasari ya somo hilo kuanzia Elimu ya Msingi hadi Kidato cha Sita. 
 
Akizungumza na Wandishi wa Habari jijini Dodoma leo, Prof Ndalichako amesema wanategemea kazi ya kuandika vitabu itakamilika Machi mwaka huu kisha kuanza uchapishaji hivyo kuwa na mategemeo ya somo hilo kuanza kufundishwa katika muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai mwaka huu. 
 
" Leo tumemsikia Rais akiwa Morogoro nimuombe radhi kwa kuchelewa lakini nimhakikishie kuwa maelekezo yake tunayafanyia kazi kwa uadilifu na kazi iliyopo sasa hivi ni kuandaa vitabu, tunajua jinsi gani anatamani kuona vijana wa kitanzania wanafundishwa somo la Historia na sisi kama wizara tunamhakikishia kuwa litaanza kufundishwa kwa uweledi mpana. 
 
Tayari tumeshaandaa mihutasari ya kufundishia kuanzia Shule ya Msingi Darasa la Kwanza hadi Darasa la Saba, Kidato cha Kwanza hadi cha Nne na Kidato cha Tano na Sita," Amesema Prof Ndalichako. 
 
Katika agizo lake la kuanzisha somo hilo la Historia, Rais Magufuli alisema litalenga kujenga uzalendo kwa vijana wa kitanzania, kulinda rasilimali za Taifa lao, kujua jinsi gani wakoloni walikua wakilaghai mababu zetu na mapambano ya Tanzania katika ukombozi wa Nchi za Bara la Afrika. 
 
" Kazi hii ya kuandaa mihutasari ya somo hili tumeshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wanahistoria na wadau binafsi, somo hili litafundishwa sambamba na somo la Historia lililopo lakini hili litakua somo la lazima," Amesema Prof Ndalichako. 
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilipo amesema madarasa ya mtihani ya Kidato cha Nne na Sita yatalisoma bila kulifanyia mtihani kwa mwaka huu lakini wale wa kidato cha pili watalifanyia mtihani huku akisema pia litafundishwa kwa lugha ya kiswahili kwa Shule zote za Msingi na Sekondari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad