HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 5, 2021

IOM YAIPONGEZA TANZANIA KWA KUWASAMEHE RAIA WA ETHIOPIA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akisalimiana Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika alipomtembelea Mhe. Waziri ofisini kwake jijini Dodoma.

 SHIRIKA la Kimataifa la Uhamaji (IOM) limeipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua iliyochukua ya kuwaachia huru Raia 1789 wa Ethiopia waliokuwa wakishikiliwa kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Pongezi hizo zimetolewa na Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa IOM Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ofisini kwake jijini Dodoma.

Bw. Mohamud amesema kitendo kilichofanywa na Rais Magufuli hivi karibuni ni cha kuigwa na kupongezwa na mataifa mengine kwani uhamaji wa watu umekuwepo kwa miaka mingi kwa ajili ya kutafuta maisha amani na usalama wao.

“Tunashukuru sana na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kitendo cha kuwaachia huru raia 1789 wa Ethiopia waliokuwa wakishikiliwa, kitendo hicho ni cha mfano na kinapaswa kuigwa na mataifa mengine,” alisema.

Viongozi hao pia wamezungumzia namna ya kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya IOM na kuzijengea uwezo taasisi na mashirika wa kukabiliana na masuala ya uhamaji ikiwa ni pamoja na kusaidia kituo cha mafunzo ya uhamaji cha IOM kilichopo mjini Moshi kuwa kituo cha Umahiri cha masuala ya uhamaji katika bara la Afrika.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi ameishukuru IOM kwa kuipongeza Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano kwa Shirika hilo katika kutekeleza kazi zake hapa nchini.

Amesema Uhamaji sio jambo linalokataliwa na nchi ila kinachotakiwa ni kufuata sheria na taratibu za nchi husika na kuongeza kuwa Kitendo hicho kitawafanya Waethiopia hao kurejea nchini kwao na kushiriki harakati za kiuchumi na hivyo kuiletea maendeleo nchi yao.

Prof. Kabudi ameiahidi IOM kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano na kituo hicho kinachotoa mafunzo ya kuongeza uwezo wa masuala ya uhamaji kwa Bara la Afrika ili kiwe kituo cha umahiri.

Amesema Tanzania itahakikisha Kituo hicho kinatambulika na Umoja wa Afrika ili kiweze kupata misaada ya kifedha na kitaalamu na hivyo kukamilisha azma ya IOM ya kuwa na kituo cha umahiri katika masuala ya uhamaji wa watu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Ameitaka IOM kuelekeza nguvu katika kusaidia nchi zenye machafuko na hali mbaya za kiuchumi na kuongeza kuwa Shirika ka IOM lazima lijikite katika kuwafanya Waethiopia waone kuwa hakuna faida kwa kuikimbia nchi yao na kwenda Afrika Kusini na kwingineko duniani na kwamba wanatakiwa kubaki nchini mwao ili kuijenga nchi yao.

Hivi karibui Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na Rais Sahle –Work Zawde wa Ethiopia Chato mkoani Geita alitangaza kuwaachia huru raia zaidi 1700 waliokuwa wakishikiliwa kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad