...Washindi 424 wa kila wiki, mwezi wazoa zawadi za mamilioni
KUELEKEA droo kuu 'Grand Finale' ya Kampeni ya NMB MastaBATA, Benki ya NMB imewataka wateja wake kuongeza kasi ya matumizi na manunuzi kwa njia ya Kadi za Mastercard na Mastercard QR, ili kujiongezea nafasi ya kushinda safari ya utalii wa ndani ama zawadi mbadala.
NMB MastaBATA inayolenga kuhamasisha matumizi na manunuzi kwa njia ya kadi, ilizinduliwa Novemba 24 mwaka jana, ambako katika kipindi cha miezi mitatu sasa, imewazawadia washindi 400 wa kila wiki, pamoja na washindi 24 wa kila mwezi na sasa wanasakwa washindi wa fainali kuu.
Wito huo umetolewa na Meneja Mwandamizi wa Biashara ya Kadi wa NMB, Manfred Kayala, wakati wa droo ya wiki ya 10 ya NMB MastaBATA, iliyofanyika chini ya uangalizi wa Joram Mtafya, Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), ambako washindi 40 walipatikana.
Kayala alibainisha kuwa, tayari washindi 400 wa kila wiki wameshazawadiwa pesa zao (Sh. 100,000 kila mmoja), kwa nyakati tofauti (jumla kuu ikiwa ni Sh. Mil.40), huku washindi wa kila mwezi 24, wakizoa zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh. Mil. 57.6.
"Washindi 12 wa kila mwezi, wao walikuwa wakijishindia zawadi mbalimbali zilizogawanywa katika makundi matatu, kila moja likiwa na thamani ya Sh. Mil. 2.4. Wito wetu sasa ni kwa wateja kuchangamkia zawadi kuu ya utalii wa ndani kwa kila mshindi na mwenza wake," alisema Kayala.
Aliongeza kuwa, kundi la kwanza la zawadi za washindi wa 12 wa mwezi ni simu janja 'smartphone' ya Samsung Galaxy Note20, huku kundi la pili lenye zawadi zenye thamni hiyo likijumuisha zawadi za friji dogo, water dispenser, Microwave na simu aina ya Samsung A21.
Kundi la tatu lilikuwa na zawadi za runinga iliyolipiwa DSTV miezi mitatu, laptop na simu ya Samsung A21, wakati washindi wa 'Grand Finale' watafanya utalii wa ndani katika mbuga za Serengeti, Ngorongoro ama visiwa vya Zanzibar, iliyolipiwa gharama zote na NMB.
"Washindi hao watakuwa huru kuchagua zawadi mbadala zenye thamani ya Sh. Milioni 8 kwa kila mmoja, ambazo ni runinga kubwa inchi 55 iliyolipiwa kisimbuzi cha DSTv kwa miezi mitatu, friji kubwa, kompyuta mpakato yaani laptop, 'microwave', 'water dispenser' na simu ya Samsung," alisema.
Meneja Huduma za Kadi wa Benki ya NMB, Ednamamu Mshubi akizungumza kwa simu na mmoja wa washindi wa droo ya kumi ya Mastabata iliyochezeshwa jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja Mwandamizi wa Biashara ya Kadi wa Benki ya NMB, Manfredy Kayala na kushoto ni Msimamizi wa michezo ya kubahatisha kutoka Bodi ya Michezo ya kubahatisha, Joram Mtafya.
No comments:
Post a Comment