HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 8, 2021

NAIBU WAZIRI BASHE AAGIZA TAKUKURU KUANZA UCHUNGUZI UPOTEVU WA MILIONI 150 ZA AMCOS YA CHABUMAA

 

 

Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe akitazama bwawa la kuhifadhia maji katika shamba la zabibu la CHABUMA AMCOS wakati wa ziara yake leo tarehe 7 Januari, 2021 katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino Dodoma kulia kwake ni Mwenyekiti wa AMCOS hiyo Bwana Gulavile Chikamanjenzi

Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe akimsikiliza Mhandisi Raphael Laizer kutoka Tume ya Umwagiliaji Dodoma ambaye alikuwa akitoa maelezo ya namna ya kuifanyia ukarabati miundombinu ya umwagiliaji wa matone katika shamba hilo.

Wawakilishi wa Wakulima wa CHABUMA AMCOS wakimsikiliza Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akiwahutubia shambani hap oleo tarehe 07 Januari, 2021.

Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe akiwa pamoja na Mkuu wa wilaya ya Chamwino Bi. Vumilia Nyamoga pamoja na Mrajis Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege katika shamba la Wakulima wa CHABUMA AMCOS.

Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe akitazama mashine za kusukuma maji kutoka visimani kwenda kwenye bwawa la kuhifadhia maji katika shamba la zabibu wakati wa ziara yake leo tarehe 7 Januari, 2021 katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino Dodoma kushoto kwake ni Mwenyekiti wa AMCOS hiyo Bwana Gulavile Chikamanjenzi akitoa maelezo.

…………………………………………………………………………………………………

Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe  ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Chamwino kuanza mara moja uchunguzi dhidi ya Viongozi wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Zabibu (CHABUMA AMCOS) katika wilaya hiyo; Waliochukua fedha kiasi cha shilingi milioni 150 ambazo zimetumika kinyume cha utaratibu.

Naibu Waziri Bashe amefika katika kijiji cha Buigili na kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa Wakulima waliokusanyika katika shamba lao la zabubu katika kijiji cha Mwegamile kata ya Buigili halmashauri ya wilaya ya Chamwino ambapo amemwagiza Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Chamwino kuchukua hatua stahiki baada ya kuelezwa kilio hicho na Wakulima hao.

“Mhe. Mkuu wa wilaya; Naomba uchukue hatua na kwakuwa Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Chamwino yupo hapa. Hawa Viongozi wachunguzwe na hatua stahiki zichukuliwe. Tuziapate fedha za Wakulima wetu kiasi cha shilingi milioni 150.” Amekaririwa Naibu Waziri Bashe.

Wakulima hao wamemwambia Waziri Bashe kuwa CHABUMA AMCOS ilipokea fedha hizo kutoka kwa Kampuni ya ARCO Vintage mwaka 2020 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya sehemu ya shamba hilo ili Kampuni hiyo iendelee kununua shehena ya zabibu kutoka katika shamba la Wakulima hao lakini kinyume na utaratibu Viongozi hao walitumia fedha hizo kwa mambo mengine.

CHABUMA AMCOS ni Ushirika wa Wakulima zaidi ya 961 ambapo imeelezwa kuwa kuanzia mwaka 2010 kwa hiari yao walianzisha shamba la zabibu lenye ukubwa wa hekari 296 ambapo walipata mkopo wa bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji pamoja na uwekezaji mwengine ambapo ulichangia shamba hilo kufikia uzalishaji wa juu wa zao la zabibu mwaka 2013 kiasi cha tani 600.

Tangu mwaka 2017 uzalishaji wa zabibu katika shamba hilo uliendelea kushuka na kusababisha Wakulima kutelekeza mashamba yao na kusababisha uzalishaji kusimama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo adhabu ya riba kutoka Benki ya CRDB kuendelea kuongezeka, kupungua kwa mapato kwa Wakulima pamoja na kukosekana kwa uongozi thabiti pamoja na usimamizi duni.

Katika kukabiliana na hali hiyo Naibu Waziri Bashe ametoa maelekezo kadhaa ili kurejesha hali ya uzalishaji katika shamba hilo.

Naibu Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji kupeleka Wahandisi kuanzia kesho tarehe 8 Januari, 2021 ili washirikiane na Wahandisi wa halmashauri ya Chamwino kufanya tathmini ya gharama ya miundombinu ya umwagiliaji na kuiwasilisha mara moja kwake.

Agizo lingine ni Timu hiyo ya Wahandisi kufanya tathimini kama Mradi huo huo unaweza kutumia nishati ya jua (Solar system) katika kuendesha mashine za kuvuta maji yanayotumika katika kilimo cha umwagiaji katika shamba hilo.

Waziri Bashe ameagiza kila Mkulima ahakikishe anasafisha kipande cha shamba lake ndani ya shamba hilo; Kazi hiyo inatakiwa kukamila ndani ya siku thelathini kuanzia leo (Tarehe 7 Januari, 2021).

Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) imeagizwa kufanya tathmini ya idadi kamili ya miche ambayo itahitaji kwa ajili ya kupandwa baada ya sehemu kubwa ya miche mingi kufa na wakati huohuo TARI inatakiwa kuanzisha kitalu cha miche ya zabibu ambapo miche hiyo itatolewa bure kwa Wakulima wenye uhitaji wa miche hiyo.

Mhe. Bashe amemtaka Mkuu wa wilaya kufanya mawasiliano na Meneja wa Shirika la Ugavi wa Nishati ya Umeme (TANESCO) wilaya ya Chamwino kurejesha huduma umeme katika shamba hilo kwa kuweka ‘transformer’ kama ilivyokuwa awali. 

Agizo lingine ni Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanda mafunzo ya namna ya kuendesha Ushirika imara na endelevu kwa Wakulima wa CHABUMA AMCOS ndani ya siku thelasini kuanzia leo (Tarehe 7 Januari, 2021).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad