MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme amewapongeza
Wakurugenzi watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kusimamia ukusanyaji
wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo Halmashauri zote nane zimevuka asilimia 80 na kufanya Mkoa kuwa katika nafasi
nzuri Kitaifa.
Mndeme pia ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa
wa Ruvuma kwa kufanya kazi nzuri ya kukusanya Mapato ya ndani ya Mkoa katika kipindi cha mwaka 2019/2020 na kuweza
kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 15 sawa na asilimia 94.
“Naipongeza Halmashauri ya Tunduru kwa kukusanya Mapato ya Ndani kwa asilimia
121.87,pia naipongeza Halamashauri ya Manispaa ya Songea tangu imeanza kutumia stendi kuu ya Shule ya Tanga
Januari1,2021 imeongeza mapato kutoka
shilingi 200,000 mpaka 970,000 kwa siku”,alisema.
Mndeme amesema Mkoa unatarajia kuimarika kiuchumi kwa
kuongezeka kwa mapato yatokanayo na kodi pamoja na ushuru kwasababu Barabara ya
Ushoroba wa Mtwara imefunguka na kupelekea
kutoa fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi.
Hata hivyo amesema biashara ambazo zinapatikana maeneo
mengine Nchi Jirani za Malawi na Msumbiji yanaunganishwa kwa kupitia usafiri wa
Ndege kupitia Uwanja wa ndege wa Songea na barabara ya lami ya Mtwara corridor.
Amesema Meli katika Ziwa Nyasa zimeanza kazi za Usafirishaji
baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Meli ya abiria ya MV Mbeya II Januari 5,2021 na Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa
ambayo inabeba abiria 300 na Mizigo tani
200.
Hata hivyo Mndeme amewaagiza Wakurugenzi kusimamia Mapato
yatokanayo na Kodi pamoja na Ushuru amesema fedha hizo hutumika katika kujenga
miradi ya maendeleo ikiwemo vituo vya Afya,Barabara,Ununuzi wa Ndege,Ujenzi wa
Reli na huduma nyingine za kijamii.
Ameziagiza Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kubuni na
kupanua wigo wa mapato kwa kuhimiza watu kudai Risiti na wafanyabiashara kutoa risiti kila wanapouza bidhaa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment