Charles James, Michuzi TV
SERIKALI
imepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Taasisi ya Hospitali ya
Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma katika kuwahudumia na kuboresha
afya za watanzania hasa waishia mkoani Dodoma na Kanda ya Kati kwa
ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Afya Maendeleo ya
Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima wakati akizindua Idara
ya Magonjwa ya Saratani, Huduma za Patholojia na Mkataba wa Huduma kwa
Watena leo jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi
huo, Dk Gwajima ameipongeza Hospitali ya Benjamin kwa namna ambavyo
imekua mstari wa mbele katika kuwahudumia watanzania pamoja na kuzindua
mkataba wa huduma kwa wateja huku akizitaka Hospitali zingine, Vituo vya
Afya kuiga mfumo huo ambao utawezesha kupata maoni yatakayoweza
kuwasaidia kutoka kwa wananchi.
Dk Gwajima amesema kwa mujibu wa
takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia tafiti za
Saratani (IARC) zinaonesha kuwa Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya
wa saratani wapatao 5,000 na inakadiriwa ifikapo 2030 kutakua na
ongezeko la wagonjwa kwa asilimia 50 hivyo kitendo cha kuzinduliwa kwa
Idara hiyo ya Saratani katika Hospitali ya Benjamin ni muendelezo wa
Serikali katika kupambana na ugonjwa huo hatari duniani.
Waziri
Gwajima amewataka watoa huduma wote wa afya nchini kutenga muda wao
katika kutoa elimu ya ugonjwa wa saratani ili kuwawezesha wananchi kuwa
na uelewa mpana wa ugonjwa huo na siyo kusubiri hadi hali kuwa mbaya.
"
Magonjwa ya Saratani yanatibika iwapo mgonjwa atawahi katika vituo vya
afya vinavyotoa huduma hizo, zaidi ya asilimia 75 ya wagonjwa hufika
katika vituo vya afya wakiwa tayari wameshachelewa sana na kuwawia
vigumu madaktari kutibu na kuponya ugonjwa huo.
Uzinduzi wa Idara
hii hapa Benjamin na kwenye Hospitali zingine hautokua na maana kama
hatutokua tukitoa elimu ili kuwafanya wananchi kuwa kwa wataalamu kabla
ya kuchelewa lakini pia nitoe rai kwa watanzania wenzangu kuwa na
utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara," Amesema Waziri Gwajima.
Kwa
upande mwingine Waziri Dk Gwajima amesema kuwepo kwa kitengo cha
Patholojia katika Hospitali ya Benjamin ni faraja pia katika kuharakisha
matibabu kwani hapo awali ilibidi sampuli zipelekwe Dar es Salaam ili
kubaini kama ni Saratani.
Akizungumzia uzinduzi huo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin, Dk. Alphonce Chandika amesema umri
unaoathirika zaidi na Magonjwa ya Saratani ni kati ya miaka 50 hadi 69
kwa wanawake hasa Saratani ya Mlango wa Kizazi na kwa upande wa wanaume
wanaoathirika ni kuanzia miaka 70 hasa kwa Saratani ya Tezi Dume.
Dk
Chindika ameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John
Magufuli kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa na upatikanaji wa
wataalamu wabobezi ambao kwa kiasi kikubwa wamewezesha huduma za
kibingwa kupatikana katika eneo la Kanda ya Kati.
Dk Chindika
amesema tafiti zinaonesha zaidi ya asilimia 66 ya Saratani zinazuilika
endapo wananchi wangeepuka viashiria hatarishi kama uvutaji wa sigara,
unywaji wa pombe kupita kiasi, kuepuka unene, kuepuka matumizi ya
vyakula vya mafuta, kuepuka mionzi ya jua hasa kwa watu wenye ulemavu wa
ngozi pamoja na kupima afya mara kwa mara.
" Septemba 2019
Hospitali ya Benjamin ilianzisha Idara ya Magonjwa ya Saratani baada ya
kununua mashine ya kisasa inayowezesha kuchanganya dawa za saratani
(Chemotherapy Compounding Hood) ambapo dawa za kuanzia tulizipata
Hospitali ya Ocean Road na baada ya hapo tuliendelea kupata kutoka MSD.
Katika
kipindi cha Januari na Desemba 2020 Idara ta Saratani tumehudumia
wagonjwa 814 wagonjwa wapya wakiwa 531 na wagonjwa marudio ni 283 ambapo
wagonjwa 192 wametibiwa hapa kwa dawa na wagonjwa 339 wamepelekwa Ocean
Road kwani walihitaji kupata matibabu ya mionzi ambayo kwa sasa
hatuna," Amesema Dk Chandika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika akizungumza wakati wa uzinduzi wa Idara ya Saratani katika Hospitali hiyo leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga akizungumza katika uzinduzi wa Idara ya Saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa leo jijini Dodoma.
Wadau wa afya na watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma wakifuatilia uzinduzi wa Idara ya Saratani katika Hospitali hiyo leo.
No comments:
Post a Comment