Na Muhidin Amri, Songea
WAKAZI wa kijiji cha Nakahegwa wilaya Songea mkoani Ruvuma,wametoa
mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea, kurudisha
fedha kiasi cha milioni 10 ilizochukua ambazo zilitolewa kukamilisha
ujenzi wa kituo cha Afya kinachojengwa katika kijiji hicho.
Wamesema,wanazihitaji fedha hizo zilizotolewa na Serikali ili waweze
kukamilisha ujenzi huo ambao umesimama kwa muda mrefu kutokana na
upungufu wa fedha, hivyo kusababisha wananchi kuendelea kuteseka kwa
kukosa huduma za matibabu karibu na makazi yao.
Wakizungumza jana mbele ya wajumbe wa shirikla lisilo la kiserikali Roa
kupitia ufadhili wa Foundation for Civil Society unaotekeleza mradi wa
mfumo wa ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii(UUJ)yaani Social
Accountability Monitoring(SAM) unaoshugulisha na elimu ya uwajibikaji na
ushirikishwaji jamii katika miradi ya Afya wamesema, fedha hizo
zinahitajika sana kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki kama
madirisha,kujenga matundu ya choo, na kununua baadhi ya vifaa tiba.
Wamesema, wamechoka kutembea umbali mrefu kwenda Hospitali ya mkoa
Songea umbali wa km 35 kufuata matibabu wakati serikali ilishatoa fedha
kwa ajili ya kupeleka huduma za Afya katika kijiji chao.
Wamesema, fedha hizo zilichukuliwa na uongozi wa Halmashauri ya wilaya
bila kushirikishwa kamati ya ujenzi na hakuna makubaliano wala taarifa
iliyotolewa kwa wananchi, jambo linalotia hofu juu ya usalama na
matumizi sahihi ya fedha hizo.
Wamemtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha fedha
hizo zinarudishwa haraka iwezekanavyo ili kukamilisha kazi zilizobaki
ili waweze kupata huduma za Afya, badala ya kwenda mbali kama Songea
mjini na vijiji jirani kufuata matibabu mara kwa mara.
Romanus Komba(63) mjumbe wa kamati ya ujenzi alisema, fedha hizo
zililetwa na Halmashauri kupitia idara ya Afya kwa ajili ya kumalizia
kazi ndogo ndogo, lakini wao kama wahusika hawakushirikishwa katika
matumizi na hazikuwekwa kwenye akaunti yoyote ya mradi bali zilibaki
katika idara ya Afya na ndiko zilikopotea.
Alisema, katika kikao cha mwisho kati ya uongozi wa Halmashauri na
wajumbe wa kamati ya ujenzi, Halmashauri ilihaidi kurudisha fedha hizo
lakini mpaka sasa bado hazijarudishwa.
Alisema, kila wanapofuatilia katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji na
kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya wanapewa majibu yasio ridhisha
na kukatisha tamaa, na kuiomba ofisi ya Mkuu wa mkoa kuingilia kati
suala hilo.
Mary Mbawala,alisema, fedha hizo zikipatikana haraka kuna uwezekano
mkubwa kazi ya ujenzi kukamilika na wananchi watapata matibabu jirani
badala ya kwenda maeneo mengine kufuata huduma ya matibabu.
Alisema, wanaopata tabu zaidi ni akina mama hasa wajawazito kwani pindi
wanapata uchungu wanashindwa kwenda kujifungua katika kituo hicho kwa
kuwa hakijakamilika na baadhi ya vyumba vinavyotumiwa na wauguzi kutoa
baadhi ya huduma hakuna faragha(usiri).
Alisema, badala yake wajawazito wanalazimika kwenda hadi Songea au
Hospitali ya Misheni Peramiho kwa ajili ya kujifungua na kufuata huduma
nyingine muhimu.
Boniventura Komba alisema, katika mradi huo kuna matatizo mengi
yaliyotokea ikiwemo fundi aliyepewa jukumu la kujenga nyumba ya
mtumishi kutoroka bila kukamilisha kazi na kuiomba Halmashauri ya wilaya
kumsaka fundi huyo ili aweze kumaliza ujenzi kwani ndiye iliyemtafuta
na sio kamati ya ujenzi.
“tulikaa kikao kilichohudhuriwa na Mbunge Jenista Mhagama na viongozi wa
Halmashauri wakiongozwa na mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri Rajabu
Mtiula, katika kikao kile Jenista aliagiza kurudishwa fedha na kutafutwa
fundi aliyekimbia, halmashauri walihaidi kutekeleza maagizo
hayo”alisema.
Hata hivyo wao kama wajumbe wa kamati ya ujenzi wanasikitika kuona
viongozi hao wamebadilika na kuwaagiza wamsake fundi ambaye hawamfahamu
kwani aliletwa na Halmashauri na sio kamati.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Dkt
Geofrey Kihaule alikiri kuwepo kwa suala hilo ambapo alisema,
Halmashauri walitenga fedha za nyongeza shilingi milioni 10 kwa ajili
ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa kituo,kumalizia nyumba ya mtumishi,
kuingiza maji pamoja na umeme.
Alisema, kati ya fedha hizo shilingi milioni mbili wamezitumia
kununua thamani za ofisini kwa ajili ya kituo, na walishindwa kuzipeleka
fedha zote kutokana na changamoto ya mahitaji ya vituo vingine
vilivyotakiwa kufunguliwa wakati ule ikiwemo Hospitali ya wilaya iliyopo
kijiji cha Mpitimbi kata ya Mpitimbi.
Dkt Kihaule alisema, kuna fedha ambazo wanategemea kupata mwezi
Januari na mara zitakapofika ujenzi wa kituo hicho utafanyika na
kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati huu ambapo Halmashauri iko
katika hatua ya mwisho kukamilisha ujenzi wa kituo hicho na vituo
vingine vya afya vinavyojengwa katika halmashauri hiyo.
Alisema, wana matumaini makubwa ifikapo mwezi Januari mwakani huduma za
Afya katika vijiji mbalimbali katika halmashauri hiyo zitaimarika na
kuwataka wananchi waendelea kuunga mkono juhudi zinazo fanywa za
kuimarisha huduma hizo.
Akiongea kwa njia ya simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Simon
Bulenganija alisema, fedha hizo zilichukuliwa kipindi cha tishio la
ugonjwa wa Corona ili kununua vifaa na pindi Halmashauri itakapokuwa na
hali nzuri, fedha hizo zitarudishwa ili ziweze kufanya kazi
iliyokusudiwa. Katibu wa mradi wa Sam unaoshughulika na kutoa elimu kwa wananchi wa kata tano katika halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma juu ya Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa jamii miradi ya Afya kufahamu kama fedha zinazotolewa na Serikali kupitia mfumo wa force Akaunti wananchi wamehusishwa na wamewajibika akiongea na wananchi wa kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini wilayani Songea. Picha zote na Mpiga na Muhidin Amri
Wednesday, December 23, 2020
WANANCHI WATOA MWEZI MMOJA HALMASHAURI YA SONGEA KURUDISHA FEDHA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment