HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 14, 2020

JESHI LA POLISI LAZUNGUKA MITAANI DAR KUWAHUDUMIA WANAONYANYASWA KIJINSIA

 

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bi. Janeth Magomi (kushoto) akizungumza kwenye zoezi la utoaji wa huduma za mkono kwa mkono zinazotembea, maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zilizoanza kutolewa Wilaya ya Kipolisi Chanika jijini Dar es Salaam juzi. Katikati ni Mkurugenzi wa Mradi katika taasisi ya Friedrich Naumann Foundation for Freedom, East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai pamoja na Mratibu wa ‘one stop center’ katika Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dk. Christina Onyango.



Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mwanamke na Mtoto katika Manispaa ya Ilala, Angella Mang’enya akizungumza katika hafla hiyo.

Huduma za mkono kwa mkono zinazotembea, maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zikitolewa Wilaya ya Kipolisi Chanika jijini Dar es Salaam. Huduma hizi ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoanza Novemba 25 na kuhitimishwa Desemba 10, 2020.

Huduma za mkono kwa mkono zinazotembea, maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zikitolewa Wilaya ya Kipolisi Chanika jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar

JESHI la Polisi nchini limewataka wananchi wanaonyanyashwa kijinsia kujitokeza katika madawati maalum yanaotoa huduma za kukabiliana na vitendo hivyo kwenye vituo mbalimbali vya Polisi. Kauli hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bi. Janeth Magomi alipokuwa akizungumza kwenye zoezi la utoaji wa huduma za mkono kwa mkono zinazotembea, maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zilizoanza kutolewa Wilaya ya Kipolisi Chanika jijini Dar es Salaam. Huduma ambayo ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoanza Novemba 25 na kuhitimishwa Desemba 10, 2020.

Akizungumza na wanahabari katika tukio hilo, Bi. Magomi alisema ni fikra potofu kudhani ya kwamba wanaokumbana na vitendo vya unyanyasaji ni wanawake na watoto pekee. Aliongeza kuwa wapo wanaume wengi wanaofanyiwa ukatili huu kwa namna mbalimbali, lakini kutokana na mfumo dume katika jamii kuamini kwamba mwanaume ni kichwa cha familia, wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa hizo.

“...Hii inatokana na mila na desturi ndiyo maana tunasema hata nyie wanaume mnaofanyiwa vitendo hivi njooni polisi tuna madawati na wataalamu wenye weledi; mtahudumiwa vizuri na haki itatendeka. Lengo letu kufanya haya ni kuhakikisha tunaendela kumlinda huyu mwanamke na mtoto na kama ilivyo kazi ya Jeshi la Polisi, kumlinda kila raia dhidi ya uhalifu wowote ukiwamo ukatili wa kijinsia kama ubakaji, ulawiti, vipigo, matusi, udhalilishaji, rushwa ya ngono, vitisho na kunyimwa huduma muhimu za kijamii,” alifafanua Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bi. Magomi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mwanamke na Mtoto katika Manispaa ya Ilala, Angella Mang’enya, alibainisha kuwa vitendo vya watoto kuzurura mitani na kuishi katika mazingira hatarishi, ni tatizo linalokua na kuhitaji nguvu ya pamoja kulikomesha.

“Wanajamii tusijue kuzaa, lakini tukashindwa kulea; lazima tuwaangalie watoto ili wasikimbilie mijini ambako wanapata masaibu mengi,” alisema.

Kwa upande wake, mwanzilishi na Mratibu wa ‘one stop center’ katika Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dk. Christina Onyango, alibainisha kuwa huduma hizo  zinazopatikana na kutolewa mahali pamoja kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia zinasaidia kupunguza urasimu na kuwajengea uwezo pia waathirika wa vitendo hivyo namna ya kutambua, kuzuia na kutoa taarifa ili hatua za haraka zichukuliwe lengo likiwa ni kuhakikisha ukatili unazuilika mapema na si kusubiri hadi utokee.

“...Katika vituo hivi, huduma zote za polisi; ujazwaji wa PF 3, huduma za daktari, unasihi kutoka maofisa wa ustawi wa jamii na mwanasheria hupatikana sehemu moja ili kumwondolea mwathirika usumbufu wa kuzitafuta maeneo mbalimbali kwa kutumia muda na pesa nyingi huku madhara yakiongezeka. Kwa siku mbili huduma za 'one stop center mobile' zitakuwa hapa Chanika, kisha itahamia Pugu tena kwa siku mbili, Gongolamboto kwa siku mbili, Segerea tena kwa siku mbili, Kiwalani, Vingunguti na Buguruni vivyo hivyo; kama alivyobainisha Afande RPC Magomi.

Aidha Dk. Onyango aliwataka waathirika kujitokeza ili kupata huduma kwa pamoja bila kujali ni kutoka jinsia gani na hata kama wanaume wanaofanyiwa ukatili huu wapo wajitokeze kupata huduma. 

Naye, Mkurugenzi wa Mradi katika taasisi ya Friedrich Naumann Foundation for Freedom, East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai, alisema ili kukomesha ukatili wa kijinsia, ni wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa kila anapobaini hali hiyo hata kama waathirika si ndugu zake.

“Hata kama si mtoto wako, ukiona anafanyiwa ukatili kwa mfano kufungiwa ndani, kupigwa kiasi cha kumwathiri, amebakwa, amelawitiwa au kufanyiwa ukatili mwingine, toa taarifa kwa Jeshi la Polisi hata kwa siri,” alisema Veni na kuongeza kuwa; “Changamoto kubwa katika vita hii ni mila na desturi kandamizi ambazo kama mtoto wa kike akifanyiwa, tunasema, lakini kama ni wa kiume, inakuwa siri… Hatuwatendei haki…”


Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kipolisi Chanika waliojitokeza kupata huduma za mkono kwa mkono zinazotembea, maarufu ‘One Stop Center Mobile’ wakisubiri kuhudumiwa.


Mwimbaji wa nyimbo za Injili Tanzania, Catherine Lukindo maarufu Dk Yatosha (wa pili kushoto) akitoa burudani katika hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad