HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 15, 2020

DAWASA HAKIKISHENI MNAONGEZA MIKOA YA KUHUDUMA WANANCHI WAPATE MAJI - WAZIRI AWESO

Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameutaka uongozi wa  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza mikoa ya kihuduma ili kuwafikia hadi wananchi wa pembezoni mwa mji.

Hayo ameyasema wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji wa Mkuranga, na kuitaka Dawasa kuongeza mikoa kutoka 15 na iwe mingi zaidi.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Aweso ameupongeza uongozi wa Dawasa chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wana mkuranga wanapata maji safi na salama.

"Dawasa mnafanya kazi kubwa sana, kwa sasa mna mikoa 15 ya kihuduma,  mnatakiwa kuongeza mikoa ya kihuduma ili muwafikie hadi wananchi wa pembezoni msitoe huduma maeneo ya mjini tu," amesema Aweso.

Aweso amesema Dawasa wanafanya kazi kubwa sana, watambue maji hayana mbadala na baada ya kuwakabidhi mji wa Mkuranga wameanza kuona uelekeo na wahakikishe wana Mkuranga wanapata maji safi na salama.

"Mradi huu mnasema hadi mwezi wa pili utakuwa umekamilika Phase 1, Dawasa kama mnaweza kuongeza nguvu hata ikiwezekana mwezi wa kwanza nije kuuzindua wana Mkuranga waanze kupata maji,"  Aweso

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga  Filberto Sanga ameishukuru Dawasa kwa jitihada kubwa wanazozifanya za kuhakikisha tatizo la maji ndani ya Mji wa Mkuranga linafikia tamati.

Mradi wa maji Mkuranga - Vikindu  unatarajia kumaliza mwanzoni mwa mwaka 2021 ukiwa  na thamani ya Bilion 5.5 za kitanzania  utakaohudumia wakazi 25,500.

Ujenzi huo unahusisha ujenzi wa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa Lita milioni 1.5, kituo cha kusukumia maji. (Booster pump station) chenye uwezo wa kusukuma maji lita 6 kwa saa na kulaza mtandao wa bomba za kusambaza maji wa Km 63.5 kwa Phase 1.

Mradi huo unatumia chanzo cha maji kutoka kisima namba HB EB 4B chenye kina cha 545m na uwezo wa kutoa maji lita 284,400 kilichopo eneo la Mkwali tumbo Mkuranga Mjini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelezo ya mradi wa Mkuranga Phase I kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso wakati wa ziara yake ya kutembelea  mradi huo unaotarajiwa kumaliza mwezi Februari 2021.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelezo ya chanzo cha maji cha mradi wa maji  Mkuranga Phase I kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso. Waziri Aweso amefanya  ziara  ya kutembelea  mradi wa maji Mkuranga Phase 1 unaotarajiwa kumaliza mwezi Februari 2021.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akikagua ujenzi wa kituo cha kusukumia maji ( booster pump)  kitakachokuwa na uwezo wa kusukuma maji Lita Milion 6 katika mradi wa maji Mkuranga. Awesu amefanya ziara ya kutembelea mradi wa maji Mkuranga unaotarajiwa kumalizika Februari 2021.
Mkuu wa Wilaya Mkuranga Filberto Sanga (katikati) akieleza jambo kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji wa Mkuranga - Vikindu unaotarajiwa kumalizika Februari 2021.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad