HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 14, 2020

CHANJO ZA MIFUGO UHAKIKA NCHINI

 


Na.Ashura Mohamed,Arusha.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Pauline Gekul ameagiza kuandaliwa kwa mkakati shirikishi wa kupeleka chanjo kwa wafugaji kuanzia mwezi Februari Mwaka 2021,kupitia programu za chanjo ya magonjwa muhimu zitakazosimamiwa na wizara.

Ameyasema hayo wakati akifunga kikao cha 38 cha  Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA),kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020,ambapo alisema kuwa zitasimamiwa na wizara hiyo.

“Hizi programu zitasimamiwa na wizara na siyo kuiachia halmashauri kwani wao hawana uwezo wa kutekeleza majukumu haya muhimu, hivyo kwa kuwa wizara imeshatayarisha kalenda ya chanjo na bei elekezi licha ya mapungufu machache yaliyopo"alisema Gekul

Aidha amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kuandaa  mkakati shirikishi na kupeleka chanjo kwa wafugaji kuanzia mwezi Februari, mwaka 2021.

Naibu Waziri Gekul amesema kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Mwaka 2003 serikali inapaswa kuhakikisha ina madaktari wa mifugo katika mikoa na halmashauri,kwa kutambua kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na ukosefu wa madaktari wa mifugo kwa mikoa 10 na halmashauri 77,.

Pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na halmashauri husika itawasilisha mapendekezo ya ikama ya watumishi kwa Utumishi kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022, lengo ikiwa ni kuhakikisha watumishi hawa wanaajiriwa ili kusimamia vizuri tasnia ya wanyama

Kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika Sekta ya Mifugo nchini Naibu Waziri Gekul amesema atamshauri Waziri wa Mifugo na Uvui  Mashimba Ndaki kuunda kikosi kazi kishirikishi kwa ajili ya kuishauri wizara katika masuala muhimu na kumtaka Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Msajili wa Baraza la Vetarinari Tanzania, kuandaa andiko ili liwasilishwe kwa Waziri Ndaki kwa ajili ya kupata ridhaa yake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) anayemaliza muda wake Prof. Dominick Kambarage amesema mfumo wa kusimamia watumishi na Sekta ya Mifugo ni muhimu kuhakikiwa ili kuimarisha sekta hiyo ambapo Mwaka 2019 TVA na TAMISEMI walianzisha mazungumzo kwa kina namna ya kusimamia sekta na watumishi.

Naye Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli akizungumza kando ya kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA), amesema baraza limejadili pia maadili kwa wataalam mbalimbali wa mifugo ambao wameshindwa kutoa taarifa za magonjwa kwa idara ya huduma za mifugo kila wiki na kila mwezi, hivyo kulazimika kutoa onyo kali kwa wataalamu 9 juu ya utoaji wa taarifa.

Katika kikao hicho pia Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amezindua chanjo mpya ya kuku inayotengezwa na wanasanyansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), inayodhibiti magonjwa matatu kwa mara moja inayofahamika kwa jina la Tatumoja ambayo imefanyiwa utafiti na kutengenezwa na wanasanyansi hao wakiongozwa na Prof. Philemon Wambura na Dkt. Mirende Kichuki.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad