Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili Mahakama ya
wilaya ya Manyoni kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo kukagua shughuli
za Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi
wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni katika ziara yake mkoani Singida.
Watumishi
wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao alipowasili
kwenye Mahakama hiyo kukagua kazi za utoaji Haki. Jaji Mkuu ameanza
ziara ya siku tatu mkoani Singida.
………………………………………………………………………..
Na Lydia Churi-Mahakama, Singida
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na
Mahakimu nchini kuongeza matumizi ya njia ya usuluhishi katika
kusikiliza na kumaliza mashauri hususan mashauri yanayohusu Mirathi.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida katika
siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani humo Jaji Mkuu amesema
mashauri yanayohusu Mirathi yana changamoto nyingi hivyo njia ya
usuluhishi itasaidia kurahisisha usikilizwaji wa mashauri hayo.
Amewataka
Majaji na Mahakimu kusimamia kikamilifu kuhakikisha wale wanaofungua
mashauri hayo mahakamani wanawasilisha taarifa za mirathi na wanafunga
hesabu ili ile dhana ya kuwa msimamizi wa mirathi ndiye atakayefaidika
na mirathi na ambayo ndiyo inayochochea migogoro inaondoka.
“Tujaribu
kutumia usuluhishi kwani njia hii pia itasaidia kupunguza mashauri
mahakamani. Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inawahimiza Majaji na Mahakimu kumaliza mashauri kwa njia usuluhishi”,
alisema Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu amesema Majaji na Mahakimu wakiweza kuwaelimisha wananchi umuhimu
wa kutatua migogoro hiyo nje ya Mahakama itakuwa ni rahisi
kuyashughulikia mashauri ya aina hiyo.
Akizungumzia
suala la maadili kwa watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu amewataka
watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na kufuata
utaratibu kwani kwa kufanya hivyo watarejesha Imani ya wananchi kwa
Mhimili wa Mahakama.
Alisema
watumishi wa Mahakama ya Tanzania wenye kada za uhudumu, watunza
kumbukumbu, walinzi na wengineo ndiyo kioo cha Mahakama na endapo
watafanya kazi weledi mtazamo dhidi ya Mahakama utakuwa chanya wakati
wote.
Kuhusu
mabaraza ya Ardhi, Jaji Mkuu amesema azma ya serikali ya kuyarudisha
mabaraza hayo mahakamani bado ipo hivyo amewataka watumishi wa Mahakama
kujiandaa kuyapokea mabaraza hayo.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu kuwa makini katika
kusimamia Sheria, Kanuni na taratibu na kuhakikisha mshtakiwa
anapokamatwa anafikishwa mahakamani ndani ya saa 48. Jaji Mkuu pia
amewataka Mahakimu hao kuwakumbusha viongozi husika kuzingatia Sheria
kanuni na taratibu wanapowakamata watuhumiwa.
Alisema
lengo la ziara yake ni kuzielezea changamoto wanazokutana nazo Majaji
wa Mahakama ya Rufani wanaposikiliza mashauri. Moja ya changamoto hizo
ni mapungufu yanayojitokeza wakati wa kuwakamata watuhumiwa. Vikao vya
Mahakama ya Rufani vilianza Septemba 14, Mahakama Kuu kanda ya Dodoma na
vitamalizika Septemba 28, mwaka huu.
Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Singida ambapo atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama.
No comments:
Post a Comment