Na Said Mwishehe, Michuzi TV -Kigoma
RAIS
Dk.John Magufuli amezindua rasmi jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma
na kwamba kuzinduliwa kwa jengo hilo kutasaidia kuondoa changamoto ya
kucheleweshwa kesi kwa wananchi wa Mkoa huo.
Dk.Magufuli
amesema hayo leo Septemba 19, 2020 wakati wa uzinduzi wa jengo hilo
ambao umeshuhudiwa na Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye , ambapo
amesema kabla ya kuzinduliwa kwa jengo hilo wananchi wa Kigoma walikuwa
wakifuata huduma ya Mahakama Kuu mkoani Tabora, hivyo kulisababisha hata
haki zao kuchelewa kutolewa.
Hata
hivyo amesema kuwa kuzinduliwa kwa mahakama hiyo ni sehemu ya mkakati
wa kujengwa kwa Mahakama , nyingine katika maeneo mbalimbali nchini kwa
lengo la kusogeza huduma za kimahakama karibu na wananchi.Pia amesema
katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea kuuimarisha muhimili
wa Mahakama kwa kuongeza idadi ya majaji hadi kufikia 50, mahakimu
938.
Wakati
huo huo Rais Magufuli ametoa rai kwa Mahakama kuhakikisha wanatunza
miundombinu ya jengo hilo ambalo limejengwa kisasa na kwamba mahakama
hiyo itumike katika kutoa haki badala ya kuipindisha haki kwasababu za
rushwa."Miundombinu iliyojengwa itumike kuimarisha utoaji haki,
haitakuwa sahihi iwapo watu watanyimwa haki zao kwasababu ya
rushwa.Wananchi wa Kigoma waitumie hiyo Mahakama katka kutafuta haki
zao."
Kwa upande wake Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye amesema amekubali kufungua jengo hilo kwani ni heshima kubwa kwake.
Awali
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Hamis Jumaa amesema kuwa kukamilika kwa
Mahakama hiyo kunakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama
kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma ambapo awali walikuwa wanafuata huduma
hiyo Mkoa wa Tabora.
Amesema
uzinduzi wa Mahakama hiyo unakwenda sambamba na ule wa ujenzi wa jengo
la Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambalo nalo lililishakamilika na
kuzinduliwa.
"Jengo
hili linabeba mambo matatu muhimu, tulikotoka, tuliko na tunakokwenda
katika safari ya utoaji wa huduma za haki nchini na hasa Kigoma kwani
haikuwa kazi rahisi na hata historia ya mambo ya Mahakama inaeleza
vizuri,"amesema.
Hata
hivyo amesema jengo hilo pia litatumika kwa ajili ya Mahakama ya Rufaa
na kwamba wanatamani siku moja nchi yote kuwa na majengo ya aina hiyo
kwa mikoa ambayo imesalia.
Hata
hivyo amesema juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha
sekta ya usafiri wa barabara, reli, usafiri wa anga, umeme na mambo
mengine yamekuwa chachu katika kuchochea haki kupatikana kwa wakati
sahihi.

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na mgeni wake Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye
wakifungua kwa pamoja jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma leo tarehe
19 Septemba 2020. PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment