HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 4, 2020

Prof Msanjila: Serikali ina Matarajio Makubwa katika Sekta ya Madini

 

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imeendelea kuboresha sekta ya madini ili kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta hiyo hatua itakayosaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato nchini.

Akizungumza leo jijini Dodoma wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Serikali ina matarajio makubwa katika sekta ya madini na ndiyo maana ilirekebisha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ili kuongeza tija.

“Nina imani Baraza mtajikita kujadili namna ya kuipeleka mbele sekta ya madini kwa vile mwaka 2025 sekta hii inatarajiwa kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa,

Vilevile Serikali inaiwezesha Tume ya Madini kwa mategemeo kwamba makusanyo yataongezeka na wananchi watashirikishwa ili sekta iweze kuimarika zaidi” alisema Prof. Msanjila.

Aliongeza kuwa, lengo la Baraza hilo la Wafanyakazi ni kutoa mchango na ushauri wa namna bora ya wafanyakazi kushirishirikiana na viongozi wa Tume ya Madini katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya taasisi na nchi kwa ujumla.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alikitaka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la taasisi hiyo kutafuta njia muafaka za kutatua matatizo ya wafanyakazi kwa kushirikiana na menejimenti ya Tume ili kutunza taswira ya taasisi hiyo na kuongeza tija katika sekta ya madini nchini.

Aidha, Prof. Kikula aliongeza kuwa Tume hiyo imeendelea kuimarisha sekta ya madini nchini na kuhakikisha Serikali inapata mapato endelevu na kuvuka malengo ya makusanyo ambayo yaliyowekwa mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2018/2019 zilikusanywa shilingi bilioni 346.78 na kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 310.32 ambazo ni sawa na asilimia 111.59 na mwaka 2019/2020 jumla shilingi bilioni 528.24 zilikusanywa na kuvuka lengo la shilingi bilioni 470.35 ambazo ni sawa na asilimia 112” alisisitiza Prof. Kikula.

Mafaniko mengine ya Tume hiyo ni uanzishwaji wa masoko 28 na vituo vya ununuzi wa madini 28 pamoja na kupungua vitendo vya utoroshwaji wa madini ambapo mwaka 2018/2019 madini yenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.72 na shilingi bilioni 27.66 yalikamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini yakiwa yanatoroshwa.

Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alisema kuwa Tume ya Madini imepanga kuendesha zoezi la uhakiki wa leseni zote za madini kwa muda wa miezi miwili na kuzifuta leseni ambazo hazitakuwa zimehakikiwa.

“Zoezi la kuhakiki leseni za madini linaanza leo Septemba 3, 2020 hadi Novemba 02, 2020, mambo ya msingi yatakayo hakikiwa ni uhalali wa leseni na leseni ambazo hazijaendelezwa wala kulipiwa ada ya mwaka zitafutwa kwa mujibu wa sheria” alisema Prof. Manya.

Prof. Manya aliongeza kuwa Tume hiyo inawataarifu wamiliki na waombaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini kurekebisha mapungufu ya maombi yao ndani ya kipindi cha siku 30, ambapo maombi yaliyopo ya wachimbaji wa kati ni leseni 15 na maombi 96 ya leseni za utafutaji madini.

Fauka ya hayo, Maafisa Madini Wakazi wametakiwa kuanzisha dawati la uhakiki wa leseni za madini katika ofisi zao ili kuwapunguzia adha wateja wao hatua itakayosaidia kupunguza usumbufu wakati wa kuhakiki leseni zao.

Wizara ya Madini tayari imekamilisha utungaji wa kanuni za uongezaji thamani madini za mwaka 2020, ambazo zitatumika kusafirisha madini yaliyoongezwa thamani nje ya nchi kwa mujibu wa kanuni hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad