Na Mary Gwera na Lydia Churi-Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuelezea Marehemu
Jaji Bethuel Mmilla kuwa alikuwa ni mchapakazi na atakumbukwa kwa
utendaji kazi wake wa kujitoa na ushirikiano.
Mwili
wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Bethuel
Mpakani Kasefu Mmilla umezikwa jana nyumbani kwake Goba Michungwani
jijini Dar es salaam baada ya kuagwa katika viwanja vya Karimjee na
baadaye kufanyiwa Ibada katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(K.K.K.T) Usharika wa Mwenge jijini Dar es salaam.
Akizungumza
katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla aliyefariki usiku
wa Septemba 24, Jaji Mkuu alisema wasifu wa marehemu Jaji Mmilla ni
mfano mzuri wa namna alivyowatumikia zaidi walio wengi kuliko
alivyojitumikia kwa maslahi yake binafsi au maslahi ya familia yake.
“Wasifu
wake unaonyesha kuwa kila kituo katika utumishi wake wa Mahakama,
amekuwa ni wa kutumikia, anayetoa, na asiye wa kutumikiwa,” alisema Mhe.
Jaji Mkuu.

Aliongeza
kuwa Maamuzi yaliyotolewa na marehemu Jaji Mmilla yatabaki kuwa mifano
hai ya mambo yote aliyoyaamini na kuyatekeleza kwa vitendo. Alisema
marehemu atakumbukwa pia kwa ucheshi na utani wake wa mara kwa mara
ambao uliwasaidia waheshimiwa Majaji wa Rufaa kusahau angalau kidogo,
maswala magumu ya kisheria na kimaamuzi.
Kwa
upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu amewashukuru madaktari, wahudumu wote
wa Hospitali ya Jeshi Lugalo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wale wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Prof. Mohamed
Janabi kwa kuwa karibu na marehemu.
Akitoa
salaam kwa niaba ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama
hiyo, Mhe. Augustine Mwarija alimuelezea Marehemu Jaji Mmilla kuwa
alikuwa ni kiongozi mwenye ushirikiano mkubwa na wenzake na aliyekuwa
akiwatia moyo katika kazi mbalimbali za utoaji haki.
Naye
Mwenyekiti wa chama cha wanasheria Tanzania (Tanganyika Law Society)
Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshalla amewashauri Majaji na Mahakimu kuandika
hukumu zenye mguso chanya katika maisha ya watu na utawala wa sheria.
“Marehemu
Jaji Mmilla aliandika hukumu nyingi ambazo zitatumika kama rejea kwa
wanafunzi wanaosoma sheria nchini, Mahakimu pamoja na Majaji” alisema
Dkt. Nshalla.

Dkt.
Nshalla pia aliwaasa familia ya marehemu kwa kuwasahuri kuishi kwa
kupendana na kushirikiana ili kuyaenzi mazuri aliyoyafanya marehemu Jaji
Mmilla.
Mazishi
ya Marehemu Jaji Mmilla yalihudhuriwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, Majaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, wadau mbalimbali pamoja na watumishi wa Mahakama.
Jaji
Mmilla alifariki dunia usiku wa Septemba 25, 2020 katika Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo kwenye Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Awali
marehemu alilazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es
salaam Septemba 23, 2020 alipokuwa akipatiwa matibabu na baadaye
kuhamishiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipofariki dunia.
No comments:
Post a Comment