HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 20, 2020

WATOTO MILIONI TANO KUSAJILIWA NA KUPATA VYETI VYA KUZALIWA KUPITIA MPANGO WA USAJILI WA WATOTO CHINI YA MIAKA MITANO

 Afisa Mtendaji Mkuu wa (RITA) Bi Emmy Hudson(katikati)akitoa taarifa ya mafanikio ya usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo hadi sasa watoto 5,400,000 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa bure.kulia kwake ni kaimu Mkurugenzi wa ulinzi wa haki za kisheria Bi Lina Msanga, mwingine ni Mkurugenzi wa TEHAMA Bw Cliff Maregeli.
 
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV 

SERIKALI kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na
Udhamini kwa kushirikiana na wadau wengine inatekeleza Mpango wa Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa kwa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ambao ni sehemu ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu.

Mpango wa Usajili wa Watoto una lengo la kuhakikisha kila mtoto aliye na umri Chini ya Miaka Mitano anasajiliwa na kupata Cheti cha kuzaliwa na vilievile kila mtoto anayezaliwa anapata nyaraka hiyo ndani ya muda mfupi baada ya tukio la kizazi kutokea. 

Taarifa ya Wakala huo kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu/ Afisa Mtendaji Mkuu Emmy Hudson amesema utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa kusogeza huduma karibu na
makazi ya wananchi kwa kutoa huduma bila malipo katika Ofisi za Watendaji Kata na Vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya Afya ya Mama na Mtoto.

Kuhusu mafanikio ya mpango wa usajili wa watoto amesema zaidi ya watoto milioni tano wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 18 ambayo mpango huo unatekelezwa na idadi hiyo kuweza kupandisha wastani wa watoto walio na vyeti vya kuzaliwa nchini kutoka asilimia 13 (kwa Mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012) na sasa kufikia asilimia 49. 

Amefafanua kati ya watoto waliosajiliwa, asilimia 50.1 ni wanaume na asilimia 49.9 ni wanawake na kuongeza mikoa inayotekeleza mpango huo ni Mbeya, Songwe, Mwanza, Iringa, Njombe, Geita,Shinyanga, Mtwara, Lindi, Mara, Simiyu, Ruvuma, Dodoma, Singida, Morogoro, Pwani, Tanga na Kilimanjaro.

Hata hivyo Mpango wa Usajili wa Watoto amesma ulianza kutekelezwa mwaka 2013 huku kasi ya usajili ikiwa ndogo wakati huo na kasi imeongezeka katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano na katika kipindi cha miaka miaka mitano mfumo umesimikwa na kuanza kutekelezwa katika Mikoa 15 na zaidi wa watoto 4,051,186 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Pia mafanikio yaliyopatikana katika awamu hii yametokana na kuongezeka kwa uwajibikaji, ushirikiano na hamasa kwa watendaji na wananchi kwa ujumla. Mpango huo umewawezesha watoto kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa ambavyo umuhimu wake unaendelea kuongezeka kutokana na kuunganishwa na upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii.

"Kutokana na mafanikio ya mpango huu, Tanzania imeweza kutambulika kama moja ya nchi inayopiga hatua katika usajili wa vizazi hata kuchaguliwa kati ya nchi tano Barani Afrika na pekee kwa Afrika Mashariki kuwasilisha mada kuhusu Mikakati na Mafanikio ya usajili yaliyopatikana katika Kipindi cha Mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu( COVID 19).
" Agosti 6, 2020 utekelezaji ulianza katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga
ambapo mpaka sasa watoto zaidi ya 387,845 wamesajiliwa na kupata vyeti katika mikoa hiyo ikiwa ni asilimia 66 ya watoto wanaotakiwa kusajiliwa. Utekelezaji katika Mikoa yote ya Tanzania Bara unategemea kukamilika mwaka 2022,"imesema Hudson.

Ameongeza kuwa wadau wanaoshirikiana na RITA katika utekelezaji wa mpango huu ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada na Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO.

Pia wapo wadau wengine muhimu wa masuala ya usajili na utambuzi wa wananchi ambao ni pamoja na Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Ametumia nafasi hiyo kufafanua kuwa mpango wa Usajili wa Watoto walio na Umri chini ya miaka mitano ni endelevu katika maeneo ambayo umeanza kutekelezwa hivyo wananchi katika Mikoa tajwa hapo juu waendelee kuitumia fursa hiyo kuwapatia watoto vyeti vya kuzaliwa mara tu wanapozaliwa.

" Tunasisitiza kwamba vyeti vinavyotolewa kupitia mpango huu ni
halali na vya kudumu na mtoto atakitumia maisha yake yote hata baada ya kuvuka umri wa miaka mitano,"amesisitiza.
Waandishi wa habari wakimsikiliza  Afisa Mtendaji Mkuu wa (RITA) Bi Emmy Hudson wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya usajili wa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad