HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 20, 2020

WAANDISHI WA HABARI ZA MAZINGIRA NCHINI WAELEZWA JITIHADA ZINAZOFANYIKA KUMALIZA MIGOGORO YA ARADHI KATI YA VIJIJI NA HIFADHI

 

 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TUME ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi imesema kwa sasa inaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kuandaa matumizi ya mipango ya ardhi kwa vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi za taifa.

Lengo ni kuondoa kabisa au kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wanyamapori na jamii zinazozunguka hifadhi hizo ili sasa waendelee kuhifadhi wanyamapori kwa ubora zaidi lakini pia kupungza chokochoko zinatokana na wananchi kuingia kwenye hifadhi za taifa na kusababisha manung'uniko,

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi Dk.Nindi Stephen wakati akitoa mada katika semina iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET)chini ya mradi wa kulinda mazingira na kukuza uhifadhi na utalii nchini Tanzania ijulikanao kwa kifupi kama mradi wa PROTECT.

Katika semina hiyo ambayo imeshirikisha wadau mbalimbali pamoja na waandishi wa habari za mazingira nchini ambao wamepata fursa ya kuelezwa hatua zinazochukuliwa ili wanyamapori na mazingira yanawazunguka yanaendelea kulindwa na kutunzwa.

Hivyo Dk.Stephen amefafanua tume hiyo na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira wameamua kufanya kazi kwa pamoja.

"Tunafanya kazi na TANAPA kuandaa matumizi ya mipango ya ardhi kwa vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi za Taifa nchini, hii kazi tumeshaianza na tumeifanya kwa kiasi kubwa, hifadhi ya Serengeti, Manyara na Tarangire timu yangu imeshamaliza kazi katika maeneo hayo.

"Tutaendelea tena katika hifadhi zilizobakia, pia tunafanya hiyo kazi kwa minajili ya uhifadhi wa wanyamapori. Hii mipaka tuliyonayo ya hifadhi ya taifa ni mipaka ya kurahisisha mifumo ya kiikolojia na kiutawala lakini haizuii wanyamapori kutoka kwenye mipaka ambayo tumeitengeneza.

"Wamekuwa na tabia ya kutoka kwenye hiyo na kwenda sehemu nyingine za hifadhi kwa kutumia korido au maeneo ya wazi wakati wanatafuta chakula kwa mifumo mbalimbali,"amesema.

Dk.Stephen amesema wakati mwingine wanyamapori wanapita katika hizo shoroba kutafuta maji au sehemu za mazalio."Kwa hiyo na maeneo haya mengi yanakuwa ya vijiji, hivyo tunashirikiana na vijiji kuandaa mifumo ya kuhifadhi wa wanyamapori kwa kutumia matumizi bora ya mipango ya ardhi".

Wakati huo huo amesema mbali ya TANAPA , wanafanya kazi pia na TFS kwa kuhakikisha wanaandaa mipango bora ya ardhi maeneo yote yanayozungukwa na misitu ya hifadhi au kwa vijiji vyote ambavyo vinahifadhi ya misitu nchini.

"Unaweza kuona ni kazi kubwa tunayoifanya kwa kushirikiana na mamlaka hizo mbili, kwa hiyo tume hii ni chombo cha kitaifa ambacho kazi yake kubwa ni kusaidiana na mashirika na taasisi nyingine kuandaa matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini,"amesema Dk.Stephen.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad