HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 28, 2020

SERIKALI YAZISHUKURU UFARANSA, NORWAY KUCHANGIA MIRADI YA UMEME VIJIJINI

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier (kulia) pamoja na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Norway hapa nchini. Kikao hicho kilichojadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati, kilifanyika Agosti 27, 2020 Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Viongozi na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakiwa katika kikao cha Waziri mwenye dhamana, Dkt Medard Kalemani na Ujumbe kutoka Balozi za Ufaransa na Norway nchini Tanzania (hawako pichani). Kikao hicho kilichojadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati, kilifanyika Agosti 27, 2020 Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe kutoka Balozi za Ufaransa na Norway nchini Tanzania, wakiwa katika kikao na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake (hawako pichani). Kikao hicho kilichojadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati, kilifanyika Agosti 27, 2020 Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam
  
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier (kushoto) na Bjorn Midthun, ambaye ni Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Norway hapa nchini. Waziri alifanya kikao na Ujumbe husika, Agosti 27, 2020 Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati.

Veronica Simba – Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania imezishukuru nchi za Ufaransa na Norway kwa mchango wake mkubwa walioutoa na wanaoendelea kuutoa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alitoa shukrani hizo jijini Dar es Salaam, Agosti 27, 2020 wakati wa kikao baina yake na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Frederic Clavier pamoja na Bjorn Midthun, ambaye ni Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

“Mmefanya kazi nzuri sana katika kutuwezesha kutekeleza miradi ya umeme vijijini. Ushirikiano wenu umetuwezesha kufikia hatua hii tuliyopo leo. Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru sana,” alisisitiza Waziri.

Akidadavua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Dkt Kalemani alisema hadi sasa zaidi ya vijiji 9,512 ambavyo ni zaidi ya asilimia 85 ya vijiji vyote 12,268 vilivyopo nchini, vimeshafikiwa na umeme.

Aidha, aliueleza Ujumbe huo kutoka Ufaransa na Norway kuwa vitongoji takribani 25,000 vimekwishafikishiwa umeme kati ya 64,339 vilivyopo nchini hivyo ameziomba nchi hizo kuendelea kutoa mchango wao katika kuwezesha kutekeleza kazi iliyobaki ya kupeleka umeme kwa vijiji na vitongoji vilivyosalia nchini.

Alisema umeme ni injini ya uchumi huku akipambanua kuwa pasipo umeme wa uhakika, haiwezekani kwa nchi yoyote kuwa na maendeleo ya kiuchumi.

Aliongeza kuwa jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Serikali hususani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, pamoja na mambo mengine, ndizo zimeiwezesha Tanzania, kuingia katika uchumi wa kati.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Balozi Clavier pamoja na Bwana Midthun, walimhakikishia Waziri Kalemani kuwa Serikali za nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha miradi mbalimbali ya umeme.

Pamoja na kueleza utayari wa kuendelea kuisaidia Tanzania, Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika kutekeleza miradi husika ambapo Waziri Kalemani amewahakikishia kuwa, ubora na uaminifu ni masuala yanayopewa umuhimu wa hali ya juu.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Styden Rwebangira, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka REA, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Balozi za Norway na Ufaransa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad