Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (aliyevaa kofia) akiangalia eneo linapojengwa Daraja la Kavunja linalounganisha Kata ya Kirando na Korongwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (aliyevaa kofia) akikagua ujenzi wa barabara za Mjini-Matai kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Km 1 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (aliyevaa kofia) akikagua sehemu iliyokamilika ya ujenzi wa barabara za Mjini-Matai kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Km 1 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Na Geofrey Kazaula
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),
Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi ambaye ni Mbuya’s Contractors
Company Limited anayejenga Barabara za Mjini-Matai katika Halmashauri ya
Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kukamilisha mradi unaotokana na Ahadi za
Mhe. Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda kulingana na
mkataba.
Mtendaji Mkuu amemuelekeza Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia
viwango katika kutekeleza mkataba huo ili barabara ziweze kuwa na ubora
unaotakiwa.
‘‘Unatakiwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati lakini pia
unazingatia viwango vinavyotakiwa, na mimi mwenyewe nitarudi hapa
kujiridhisha’’ alisema Kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff alitembelea miradi ya barabara na
madaraja katika Halmashauri mbalimbali ndani ya Mkoa wa Rukwa ambapo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alitembelea miradi ya barabara za
lami katika Mji wa Namanyere zilizokamilika na zinazoendelea kujengwa
kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa TARURA alitembelea na kujionea hali ya Daraja la
Kavunja lililopo Kijiji cha Kirando katika Halmashauri ya Wilaya ya
Nkasi mkoani Rukwa ambapo hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi
huo na jinsi ambavyo Ofisi ya Mratibu wa Mkoa wa Rukwa inavyoshughulikia
changamoto zilizo jitokeza za menejimenti ya mkataba na usanifu wa
daraja hilo. Hivyo, aliahidi kutuma Timu ya Wataalam kuja kwenye daraja
hilo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hizo.
Akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Kiongozi huyo
alitembelea na kujionea hali ya daraja la Kankwale lililopo Kata ya
Kankwale ambalo pia limeharibika kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na
kusababisha kukatika kwa mawasiliano ambapo aliagiza kuwa ujenzi wa
daraja hilo uanze mara moja kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ili kuhakikisha
huduma za usafiri na usafirishaji zinarejeshwa kwa wananchi.
Naye Kaimu Mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Selemani Mziray
amesema kuwa katika Mji wa Namanyere, ujenzi wa barabara za lami
zinazotokana na Ahadi za Mhe. Rais, hadi sasa kilomita mbili (2)
zimekamilika na kilomita moja (1) ipo katika utekelezaji na itakamilika
tarehe 30/08/2020.
‘‘Tunajitahidi ili kuhakikisha miradi hii inayotokana na Ahadi za Mhe.
Rais inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi
waweze kunufaika”, alisema Mhandisi Mziray.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Rukwa, Mtendaji Mkuu wa TARURA
alifanya kikao kazi na Mameneja wote wa TARURA waliopo kwenye
Halmashauri zote zilizopo kwenye Mkoa wa Rukwa ili kutoa maelekezo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujadili namna ya kuendelea kurejesha
mawasiliano kwa maeneo yaliyoathiriwa sana na mvua.
No comments:
Post a Comment