Mbio za hisani za Benki ya CRDB zakusanya shilingi milioni 200 kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonya ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, August 16, 2020

Mbio za hisani za Benki ya CRDB zakusanya shilingi milioni 200 kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonya ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Mbio za hisani za Benki ya CRDB zimekuwa na mafanikio makubwa kwa kukusanya shilingi milioni 200 kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo zaidi ya watu 4,000 walishiriki.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo za hisani zenye lengo la kusaidia jitihada za Serikali katika kutoa huduma bora za afya kwa watoto na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusiana na magonjwa wa moyo kwa watoto.

“Kupata huduma bora za afya ni haki ya kila binadamu, haki ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kila binadamu, hususan watoto wetu na vijana katika kukua vizuri na kuwa na afya njema,” alisema Mama Samia.

Makamu wa Rais pia aliwapongeza washiriki na makampuni yaliyoshiriki kuandaa CRDB Bank Marathon kwa kuungana kwa pamoja kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa watoto, huku akiwataka watu wote kuendeleza jitihada hizo. “Upo usemi usemao ukiokoa maisha ya mtu umeikokoa dunia, jitihada hizi zisiishie hapa, tuendelee kushirikiana na Taasisi yetu ya Moyo katika kurejesha tabasamu kwa Watoto wetu,” alisisitiza.

Akitoa hotuba yake, katikati ya shangwe na nderemo za mziki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema mbio hizo za hisani zimefanikiwa kuvuka lengo la kiwango kilicho wekwa cha shilingi milioni 200. Nsekela alisema mbio hizo za hisani zilizokuwa na kauli mbiu ya Kasi Isambazayo Tabasamu zimeweza kuwaunganisha washiriki kwa pamoja kuchangia fedha hizo zinazoelekezwa kwenye upasuaji wa moyo kwa watoto.

Nsekela alisema kwa muda mrefu Benki ya CRDB kupitia sera yake ya kusaidia jamii (CSR Policy) imekuwa ikiisaidia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kufanya upasuaji kwa watoto. Ili kuongeza ushiriki wa jamii kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwamo changamoto ya upatikanaji wa huduma bora afya kwa watoto, Benki ya CRDB imeanzisha mbio hizo za hisani ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka.
“Michezo ina nguvu ya kuwahamasisha watu kushiriki katika mabadiliko chanya. Nifuraha kubwa sana kwetu kuona mbio hizi za hisani za CRDB Bank Marathon zinachochea mabadiliko chanya katika jamii na kuongeza ushiriki wa watu katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo.

“….nimefarijika kuona watu wengi wemaungana nasi katika jitihada za kusambaza tabasamu kwa watoto wetu. Mafanikio haya tusingeyafikia isipokuwa kwa kujitoa kwao. Tunawashukuru washiriki wote na makampuni yaliyoshirikiana nasi kuwezesha kufikia lengo,” aliongezea Nsekela.

Naye Waziri wa Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni Dkt. Harison Mwakyembe aliipongeza Benki ya CRDB na wadau walioshiriki katika mbio hizo za hisani kwa mchango wao walioutoa kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto.

“Benki ya CRDB imeonyesha sio tu ni bora kwa kutoa huduma bora kwa wateja, lakini pia ipo mstari wa mbele katika kusaidia jamii kwasababu uongozi wa benki hii unaelewa taifa lolote lenye mafanikio ni lazima kuwekeza katika afya ya watoto,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe alisema Benki ya CRDB imedhihirisha kuwa wapo Watanzania ambao wanauwezo wa kuongoza taasisi kubwa nchini na kwa mafanikio makubwa huku akibainisha kuwa miaka ya nyuma mabenki mengi yalikuwa yakiendeshwa na watu kutoka nje.

“Serikali inapendezwa sana na utendaji kazi wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwasabubu mnafanya vizuri katika nyanja zote, katika biashara na katika kusaidia jamii kama hawa watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo,” alisema Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohammed Janabi alisema sasa hivi wapo 500 katika orodha ya Taasisi hiyo wanaosubiria kufanyiwa upasuaji wa moyo huku wazazi na walezi wao wakishindwa kumudu gharama za matibabu. Prof. Janabi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo za hisani huku akiwataka wadau wengine pia kujitokeza kusaidia.

“Nimeshiriki mbio nyingi lakini mbio hizi za hisani zilizoandaliwa na Benki ya CRDB ni za kipekee sana kwasababu tunapata nafasi ya kusambaza tabasamu kwa washiriki wenzangu na kwa watoto,” alisema Boniface Ngwata mshindi wa mbio za baiskeli km 42.

“CRDB Bank Marathon ni mbio ambazo zinahamasisha sana kushiriki kutokana na lengo na dhamira yake. Ushindi na tabasamu langu leo ninalielekeza kwa watoto wote ambao wanahitaji upasuaji wa moyo, Mungu awalinde na kuwafanyia uponyaji,” alisema Faulina Mathayo mshindi wa mbio za km 21 upande wa wanawake.

Mbio hizo za hisani zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi na serikali ikiwamo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ambaye aliipongeza Benki ya CRDB na washiriki wote wa mbio hizo za hisani kwa kujitoa kwao. Katika matokeo, Boniphace Ngwata alishinda mbio za baiskeli km 42 kwa upande wa wanaume na Jamila Abdul alishinda mbio za baiskeli km 42 upande wa wanawake. Joseph Panga aliibuka kidedea katika mbio za km 21 upande wa wanaume wakati Faulina Mathayo akiibuka kidedea kwa upande wa wanawake. Wahindi wa 10 kwa upande wa wanaume na wanawake ni Mathayo Yamhenda na Angelina Mboya.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad