Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameuagiza Uongozi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuboresha huduma za tiba kwa
wananchi wanaofika kupata huduma za afya katika hospitali hiyo.
Prof. Makubi ametoa maagizo hayo kufuatia ziara ya kushtukiza
aliyoifanya kwenye Hospitali hiyo na kushuhudia changamoto mbalimbali
ikiwemo baadhi ya wagonjwa kuchelewa kupewa huduma, Madaktari bingwa
kutowaona wagonjwa kwa wakati na huduma za vipimo kuchelewa.
“Yapo mazuri tumeona mnayofanya kwa wananchi na tunawapongeza, ila
lazima kuangalia upande wa pili ambao wananchi wanayataka, kwa yale
mapungufu tuliyoyaona tungependa kuona yanaboreshwa haraka ili
hospitali hii iwe ya mfano kwa hospitali zote za rufaa za mikoa kwa
kutoa huduma zilizo bora”.
Prof. Makubi amesema hospitali hiyo inatakiwa kuonesha mfano kuanzia
utoaji wa huduma bora kwa mteja pamoja, kupunguza muda wa wagonjwa
kusubiri huduma, upatikanaji wa wauguzi na mabingwa wanapohitajika na
usafi wa wodi kwani ndiyo chachu ya wananchi wengi kufika hapo na
kupata huduma kabla hawajapewa rufaa ya kwenda Hospitali kubwa kama
Benjamin Mkapa.
Aidha, Mganga Mkuu huyo ameutaka uongozi na watumishi wa hospitali
hiyo kutambua majukumu yao kwa kuonesha kuwajali wananchi wote na
kuwataka kuweka utaratibu usio na usumbufu kwa wagonjwa na kupatiwa
huduma kwa wakati.
Prof. Makubi alionyesha kusikitishwa alipokuta wodini baadhi ya
wagonjwa wamelazwa na hawajaonwa na Mabingwa kwa zaidi ya siku tatu,
wauguzi wakiwa hawajaambatana na madaktari katika kuzungukia wagonjwa
huku madaktari wa vitendo (interns) wakifanya “procedures” peke yao
bila uangalizi na baadhi ya wagonjwa wengine wakiwa wamelazwa chini
wakati vitanda viko wazi pamoja na mazingira ya wodi hayakuwa ya
kuridhisha na kukosekana kwa mpangilio wa vifaa (5S)
“Lazima watumishi mjitambue mko wapi kwani awamu hii ni ya kuwajali
wanyonge na kufanya kazi kwa bidii ndio kanuni ya awamu hii hapa kazi
tu”. Alisisitiza Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameelekeza madaktari wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa
ushirikiano na wauguzi katika kuwahudumia wagonjwa katika wodi, kuleta
mabadiliko kwa kutengeneza miongozo mbalimbali ya kusimamia huduma na
kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kila mwananchi anayefika
hospitalini hapo ahudumiwe kwa wakati na huduma inayostahili.
Kwa upande mwingine Mganga Mkuu huyo wa Serikali ameitaka hospitali
hiyo kuboresha idara ya huduma kwa wateja (Customer Care) kwani hakuna
mgonjwa anayependa kuchelewa kupata huduma hivyo lazima kutoa huduma
bora na zinazohitajika kwa wananchi wote.
Prof. Makubi ameelekeza Uongozi wa Hospitali kuhakikisha mashine za
maabara ambazo zimeishiwa vitendanishi, zinaanza kufanya kazi haraka.
"Ni vizuri mkapunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo vya damu,
X-ray, ultrasound, na Moyo na vipimo vingine".Alielekeza Prof. Abel
Makubi.
Prof.Makubi aliagiza Hospitali zote nchini zifanyie kazi changamoto
alizoziona hapo Dodoma, na akaagiza Idara ya ukaguzi wa huduma bora
kutoka wizarani wafanye ufuatiliaji wa utoaji wa huduma mikoani,
wilayani na Vituo vya afya kila mwezi na kutoa taarifa kwake.
Prof. Makubi akiangalia duka la dawa lililopo hospitalini hapo akiwa na wakurugenzi wa wizara ya Afya
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiangalia moja ya mashine zilizopo kwenye maabara ya hospitali hiyo
Mganga Mkuu wa Serikali akitazama moja ya faili la mgonjwa aliolazwa kwenye wodi hiyo ambapo alibaini mapungufu.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akikagua wodi ya wanaume iliyoko hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma.Kushoto ni Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo Stanley Mahumbo.
No comments:
Post a Comment