MAANDALIZI HUDUMA MPYA KUTIBU MFUMO WA UMEME WA MOYO ‘MBIONI’ KUKAMILIKA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 12, 2020

MAANDALIZI HUDUMA MPYA KUTIBU MFUMO WA UMEME WA MOYO ‘MBIONI’ KUKAMILIKAHuduma mpya kabisa ya kutibu tatizo la mfumo wa umeme ulioharibika kwa njia ya kisasa zaidi inatarajiwa kuanza kutolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kati ya kipindi cha kuanzia mwezi Agosti hadi Oktoba, mwaka huu.

JKCI hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ili kuanza kutoa huduma hiyo baada ya kupatiwa na Serikali kiasi cha Sh. bil 4.3 kwa ajili ya kusimika mitambo pamoja na kuanzisha chumba kingine cha tatu cha upasuaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi aliweka wazi hayo hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) ambako JKCI inashiriki kutoa huduma ya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo pamoja na elimu kwa wananchi jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo.
  
“Maandalizi yanakwenda vizuri, tunatarajia kati ya Agosti hadi Oktoba, mwaka huu, pale JKCI tutaanzisha huduma mpya kabisa, mfumo wa umeme unapoharibika tutakuwa tunaweza kuingia ndani ya moyo, tukatizama sehemu zilizoathirika na kuziunguza ama kuzifanyia marekebisho,” 

“Huduma hiyo kitaalamu inaitwa ‘Electrophysiology studies’ ni huduma ambayo haijawahi kutolewa hapa nchini na maandalizi ya kuanzisha chumba cha tatu cha upasuaji nayo yanakwenda vyema” alisema Prof. Janabi.

Aliongeza “Hapa SABASABA hii ni mara ya nne JKCI tunashiriki, mwaka jana tulipata zawadi ya kuwa banda lililotoa huduma bora kwa upande wa huduma za afya SABASABA.

“Mwaka jana banda letu lilikuwa dogo, mwaka huu tumeongeza karibu mara mbili na nusu, tangu tumeanza hadi sasa namba ya watu tulioona imeongezeka. Tumeona zaidi ya watu 1,000 na takribani watu 370 tumewakuta na Shinikizo la Juu la Damu na walikuwa hawajijui hali zao hapo kabla.

“Tumewapa rufaa kuja kwenye taasisi yetu kwa matibabu zaidi, katika banda letu tunavyo vifaa ikiwamo kipimo cha Electoral Cardiograph (ECG), tunao madaktari wa chakula kwa wanaohitajika kupunguza uzito, wanapewa elimu.

“Yupo daktari wa nasaha anatoa elimu kwanini mtu asiache kunywa dawa na pale zinapomsumbua nini cha kufanya, tunao madakrari bingwa wa udhamiri wa magonjwa ya moyo nikiwamo mimi mwenyewe.

“Tunaonesha pia vifaa kadhaa vinavyotumika wakati wa upasuaji, tunavyo vile tunavyotumia kusimamisha moyo pale inapohitajika kufanya marekebisho wakati tunafanya upasuaji,” alisema Prof. Janabi.

Aliongeza “Tunajaribu kuwaeleza wananchi waelewe, pia tulipata mgonjwa mmoja hapa Sabasaba ambaye amehangaika kutafuta matibabu, tulipompima kipimo cha Echo Cardiograph (ECHO) tuligundua moyo wake unafanya kazi chini ya kiwango cha asilimia 30.

“Ikiwa tusingemgundua hapa maana yake angeendelea kuhangaika na kutumia fedha nyingi kujitibu, kutokana na hali yale pale JKCI tunacho kifaa kinachoitwa CRTD ambacho tunaweza kumpandikiza na akaimarika afya yake na kuendelea na maisha yake kama kawaida,” alisema.

Alisema bila kupepesa maneno JKCI imekuwa na mchango mkubwa kwenye tiba ya magonjwa ya moyo ndani ya nchi na katika nchi jirani zinazotuzunguka.

“Zanzibar, Malawi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wote hawa huduma kama zetu hawana, tunawahudumia hapa JKCI.

“Rwanda tulipeleka timu yetu mbayo ilikaa wiki nzima na kafanya upasuaji kwa wagonjwa 25, hii yote tunaishukuru Serikali kwa sababu imekua pamoja nasi katika kila hatua ya kuimarisha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini,” alisisitiza.
 Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess akifuatilia huduma zinazotolewa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea banda hilo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kushoto ni Daktari kutoka JKCI Pedro Pallangyo.
Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akimwelezea Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga mwitikio wa wananchi kufanya uchunguzi wa afya ya mioyo yao katika banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad