HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 8, 2020

DKT KALEMANI AWACHARUKIA WANAOTOZA BEI KUBWA ZA UMEME


Veronica Simba – Sengerema

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, ametoa onyo kali kwa wazalishaji binafsi wa umeme, wanaowatoza wananchi gharama kubwa tofauti na bei elekezi ya Serikali.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Julai 7, 2020, Waziri alisisitiza kuwa gharama stahiki ya umeme kwa wananchi wote wenye matumizi ya kawaida ni shilingi 100 tu kwa uniti moja.

Alisema, wananchi wanapaswa kutozwa gharama inayofanana katika maeneo yote nchini kwani wote wana haki sawa.

“Bei hiyo ni kwa maeneo yote nchini vikiwemo visiwa na ni kwa umeme wa aina zote pasipo kujali ni wa TANESCO au kutoka kwa wazalishaji binafsi wanaotumia umeme jua na aina nyinginezo,” alisisitiza Waziri.

Alitoa agizo kwa viongozi wa Serikali, hususan Wakuu wa Wilaya kote nchini, kuwachukulia hatua wazalishaji binafsi wa umeme, watakaobainika kukiuka mwongozo huo wa Serikali.

Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali, hususani wanaoishi visiwani, kwamba wamekuwa wakitozwa gharama kubwa na wawekezaji binafsi wa umeme hali inayosababisha wengi wajisikie kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Waziri alisema kamwe Serikali haitavumilia tabia za aina hiyo zinazooneshwa na baadhi ya wawekezaji binafsi wa umeme kwani imewaamini kutenda haki katika kuwafikishia umeme wananchi hao ambao hawajafikiwa na gridi ya Taifa.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali inaendelea na zoezi la kupeleka umeme wa gridi ya Taifa katika visiwa vyote nchini kwa kupitisha nyaya chini ya maji yanayozunguka visiwa hivyo.

Aliwataka wananchi wa visiwani ambao hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa watulivu kwani huduma hiyo itawafikia wote awamu kwa awamu.

Akiwa katika Mkutano huo, Waziri aliagiza kukamatwa na kuhojiwa wawakilishi wa kampuni ya kuzalisha umeme wa jua iitwayo Jumeme, baada ya wananchi wa kisiwa cha Maisome wilayani humo, kuwatuhumu kuwa wamekuwa wakiwauzia umeme kwa gharama ya shilingi 3,500 kwa uniti moja.

Akizungumza katika Mkutano huo wa Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alipongeza hatua za makusudi ambazo Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imekuwa ikizichukua katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme.

Aidha, alitoa shukrani na pongezi kwa Serikali, kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, kutokana na kutatuliwa kwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara, iliyokuwa ikiwakosesha amani wananchi hao.

“Umeme sasa haukatiki tena mara kwa mara kama ilivyokuwa awali na hata inapotokea, TANESCO wanatoa taarifa kwa wakati wakieleza sababu za kukata, muda utakaotumika kurejesha huduma hiyo pamoja na maeneo yatakayoathirika,” alisema. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme wilayani humo.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Julai 7, 2020.
 Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) na wananchi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) Julai 7, 2020. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
 Mzee Julius Luzendaze, akitoa maoni yake kuhusu upatikanaji wa umeme, wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) na wakazi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Julai 7, 2020.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akieleza dhamira ya ziara yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole (kushoto), alipowasili wilayani humo Julai 7, 2020 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
 Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Dauson Kamaka (kulia) na Msimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini, Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale (kushoto), wakifuatilia Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) na wakazi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza (hawapo pichani). Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Julai 7, 2020.
Sehemu ya umati wa wakazi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipofanya ziara wilayani humo Julai 7, 2020 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad