HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 28, 2020

DKT. KALEMANI HARIDHISHWI NA KASI NDOGO YA MATUMIZI YA UMEME TABORA

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kulia) akizungumza na Mkazi wa Kijiji cha Busomeke( katikati) wilayani Igunga mkoani Tabora baada ya waziri huyo kuwasha umeme katika nyumba mwanakijiji huyo. 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Viongozi wa Kijiji cha Busomeke katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. 
Viongozi wa Kijiji cha Mizanza wilayani Igunga Mkoani Tabora wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, hayupo pichani baada ya kufanya ziara kijijini hapo ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. 

Moja ya nyumba iliyowashiwa umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani Tabora baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kufanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme Vijijini wilayani humo Aprili 27, 2020. 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati)akizungumza na Viongozi wa Kijiji cha Mizanza katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. 
Mbunge wa Manonga, Saif Gulamali (katikati) akizungumza na Viongozi wa Kijiji cha Mizanza katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. Kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

Na Zuena Msuya, Tabora
WAZIRI wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuongeza kasi ya kutumia umeme unaopatikana mkoani humo kwakuwa matumizi yao yapo chini zaidi kulinganisha na umeme unaozalishwa mkoani humo.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati akikagua shughuli za usambazaji wa umeme vijijini katika Kijiji cha Mizanza na kuwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani Tabora, Aprili 27, 2020.

Dkt. Kalemani alisema kuwa mitambo ya kufua umeme iliyopo mkoani humo inauwezo wakuzalisha Megawati 42 za umeme ili itumike mkoa mzima lakini mpaka sasa matumizi ni Megawati 14 tu.

“Kwa nini ninyi wakazi wa Tabora hamtaki kutumia umeme haliyakuwa tayari miundombinu imewafikia na bei ya kuunganisha ni 27,000 tu! mitambo ya hapa Tabora inauwezo wa kufua umeme wa Megawati 42, ninyi matumizi yenu hayafiki hata nusu ya umeme huo,hii si sawa mtaharibu mitambo yetu kwakuwa mingine italazimika kuzimwa na ikizimwa kwa muda mrefu itaharibika na nchi itapata hasara” alisema Dkt. Kalemani.

Aliwataka Viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuunganisha umeme katika nyumba zao.

Vilevile aliwataka wananchi hao kuongeza shughuli za uzalishaji mali kama vile viwanda vidogo vinavyotumia umeme ili kuongeza idadi ya matumizi ya umeme ambao mwingi hupotea kwa kukosa watumiaji hali yakuwa bado wakazi wengi hawana huduma hiyo.

Katika ziara yake hiyo, aliwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme.

Akiwa katika Kijiji cha Mizanza, Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kuharakisha upelekaji wa nguzo kijijini hapo, ili kuwapa fursa wakazi wa kijiji hicho kuunganishiwa umeme, hivyo amewataka wakazi hao kulipia gharama za uunganishwaji na kutandaza nyaya katika nyumba zao.

Aliendelea kusisitiza kuwa miradi ya usambazi umeme vijiji hauna fidia, hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa wakandarasi na TANESCO pindi wanapopitisha miundombinu katika maeneo yao kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.

Hata hivyo aliwataka kutumia wakandarasi walioainishwa na TANESCO na wanaotambulika katika serikali za mitaa na vijiji vyao ili kuepuka vishoka na watu wasiowaaminifu.

Sambasamba na hilo, aliwaeleza kuwa wasikubali kulipia miundombinu ya umeme kama nguzo, nyaya, mashineumba (Transfoma) wala mita za LUKU.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad