Waziri wa Nishati aweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi za Tanesco Chato, Geita - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 16 October 2019

Waziri wa Nishati aweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi za Tanesco Chato, Geita

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za Tanesco katika Wilaya ya Chato na Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita zitakazokuwa na hadhi ya kimkoa ya Kitanesco.

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 15 Oktoba, 2019 katika Kitongoji cha Mlimani, wilayani Chato ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka, Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Edson Ngabo na watendaji wengine kutoka Wilaya ya Chato, TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Kabla ya kuweka Jiwe la Msingi, Dkt Kalemani alipongeza juhudi za TANESCO za ujenzi wa ofisi katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa hadi sasa TANESCO ina takribani ofisi 160 kwa nchi nzima.

"Leo tunaanzisha ujenzi huu mwingine wa ofisi mbili mpya, ya Chato na Geita. Hapa Chato Tanesco ilikuwa ikipanga kwenye jengo la mtu binafsi lakini sasa kutakuwa na jengo litakalowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, lakini nitoe angalizo kuwa, lisiwe kigezo cha kukaa ofisini badala ya kuwafuata wateja kule waliko." alisema Dkt.Kalemani

Dkt Kalemani alitoa maelekezo kuwa, ujenzi wa majengo hayo ulingane na thamani ya pesa iliyotengwa na TANESCO ihakikishe  kunakuwa na wataalam wa kutosha kuhudumia wananchi mara baada ya majengo kukamilika.

Aidha, aliiagiza TBA kuhakikisha kuwa ujenzi wa majengo hayo unakamilika mwezi Aprili 2020 kama ilivyopangwa na wakati wa ujenzi wazingatie kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya ujenzi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka alieleza kuwa majengo hayo yanajengwa kwa kutumia fedha ya Serikali kupitia TANESCO huku mkandarasi akiwa ni TBA.

Vilevile alisema kuwa ujenzi wa majengo yote mawili unaanza mwezi Oktoba, 2019 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi Sita.

Katika kuimarisha utoaji wa huduma, alisema kuwa, TANESCO imekamilisha ujenzi wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini ambayo ni Songea, Kibamba, Mbezi Beach, Ifakara, Bahi, Kaliua, Igunga na Uyui huku majengo ya TANESCO wilayani Kishapu na Kyerwa yakitarajiwa kukamilika mwezi huu.

Aliongeza, ujenzi wa majengo mengine unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku ujenzi wa majengo katika Mkoa wa Kilimanjaro, Mtwara na Pwani ukitarajiwa kuanza kabla ya mwezi Disemba mwaka huu.
 Muonekano wa jengo la TANESCO wilayani Geita mara baada kukamilika ujenzi wake mwezi Aprili mwaka 2020.
 Muonekano wa jengo la TANESCO wilayani Chato, Mkoa wa Geita, mara baada kukamilika ujenzi wake mwezi Aprili mwaka 2020.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia, mbele) na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho (kushoto, mbele) wakifunua kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilayani Chato na Geita, mkoani Geita. Wengine ni watendaji kutoka TANESCO, Wakala wa Majengo (TBA) na Wilaya ya Chato.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia, mbele) na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho (kushoto, mbele) wakipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilayani Chato na Geita, mkoani Geita. Wengine ni watendaji kutoka TANESCO, Wakala wa Majengo (TBA) na Wilaya ya Chato.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akisalimiana na watendaji mbalimbali waliofika katika Kitongoji cha Mlimani wilayani Chato kushuhudia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilayani Chato na Geita, mkoani Geita.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akisalimiana na watendaji mbalimbali waliofika katika Kitongoji cha Mlimani wilayani Chato kushuhudia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilayani Chato na Geita, mkoani Geita.
 Baadhi ya wananchi, wilayani Chato wakiwa katika Kitongoji cha Mlimani wilayani Chato kushuhudia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilayani Chato na Geita, mkoani Geita.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa Ofisi za TANESCO katika Wilaya ya Chato na Geita mkoani Geita wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hizo iliyofanyika katika Kitongoji cha Mlimani wilayani Chato.  Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad