HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 October 2019

WAZIRI MKUU AMPA SIKU TATU MHAZINI ITIGI AREJESHE POSHO ALIYOJILIPA KINYUME CHA TARATIBU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa siku tatu Kaimu Mweka Hazina wa wilaya ya Itigi, Bw. Optatus Likiliwike ahakikishe anarejesha sh. milioni 1.6 ambazo alijilipa posho kinyume cha utaratibu.

“Kabla sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione pay in slip kuthibitisha kuwa fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki, niione hiyo pay in slip kabla sijaondoka," amesema Waziri Mkuu.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Oktoba 4, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Manyoni ambao wanajumuisha Halmashauri za Wilaya za Itigi na Manyoni.

"Wewe si ndiye Otto au Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?," alihoji Waziri Mkuu.

“Nilichukua fedha lakini kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa naenda wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma," alijibu Bw. Likiliwike.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka afisa huyo arejeshe sh. milioni 196 za ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.

"Hizi fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za retention, ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi nyingine?" Waziri Mkuu alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina waliokuwepo kabla yake.

Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Bw. John Mgalula ambaye aliteuliwa wiki iliyopita asimamie marejesho ya posho za Bw. Likiliwike pamoja na marejesho ya sh. milioni 196 ambazo mweka hazina huyo ameahidi kuwa Halmashauri yake imetenga sh. milioni 70 ili zirejeshwe kila mwaka.

Waziri Mkuu amesema wanapaswa kutenga fedha zaidi ili fedha hiyo iweze kurejeshwa haraka kwa Wakala wa Majengo nchini (TBA) ambaye ni mkandarasi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo.

Naye Bw. Optatus Otto Likiliwike alisema kwamba fedha zinazodaiwa kutumika zilikuwa zimetumwa na HAZINA kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini zililazimika kuchotwa na uongozi uliopita ili zitumike kuweka miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya ya Itigi.

Alisema waliohusika ukiukwaji huo ni Mkurugenzi aliyepita, Bw. Pius Luhende na Mweka Hazina aliyepita Bw. Charles Mnamba. Hata hivyo, alikiri kwamba fedha hizo hazikuombewa kibali cha matumizi hayo.

Akiweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo, Waziri Mkuu alisema anaweka jiwe hilo kwa sababu ameridhishwa na maelezo ya Meneja wa TBA kuhusu ujenzi wa jengo hilo.

Amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo wahoji matumizi ya fedha hizo na wawaorodheshe wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo. “Kaeni na mkaguzi wenu wa ndani, awape taarifa juu ya matumizi hayo,” alisema.

Pia amewataka watumishi wa umma waheshimiane na watambue Mamlaka nyingine kama za madiwani. Pia aliwataka wafuate taratibu na kanuni za utumishi na siyo wajifanyie mambo kwa holela.

Awali, Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Bw. Charles Fussi ahakikishe anarejesha mkopo wa sh. milioni 100 kutoka benki ya CRDB ambazo walikopeshwa madiwani, wakarejesha kiasi lakini Halmashuri haijazipeleka benki.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa deni hilo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu na riba zinazotozwa na benki.

“Hakikisha unamaliza hilo deni la sivyo hawa Waheshimiwa hawatapata stahili zao hadi deni liishe. Pia unataka kusababisha mgogoro baina ya benki na Halmashauri.”

Aliwataka wadiwani hao waisimamie kwa karibu Halmashauri yao. “Madiwani muiangalie Halmashauri yenu kwa kina. Hatuwezi kuendesha Halmashauri kwa utaratibu huu wa kila mmoja kufanya kazi anavyotaka.”

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Watumishi wa Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, kwenye ukumbi wa Halmashairi wilayani hapo, Oktoba 4.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad