HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 October 2019

WAZIRI MKUCHIKA NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA KLABU YA KUPINGA RUSHWA YA SHULE YA SEKONDARI MTANGALANGA WILAYANI NEWALA

Na James K. Mwanamyoto,Newala
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) na Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 Bw. Mzee Mkongea Ali, wameridhishwa na mchango wa Klabu ya Kupinga Rushwa ya Shule ya Sekondari ya Mtangalanga iliyopo Halmashauri ya Mji Newala.

Viongozi hao wamesema hayo baada ya ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2019 kuitembelea Klabu ya Shule hiyo kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia kazi za klabu hiyo, Mhe. Mkuchika amesema, akiwa kama Waziri mwenye dhamana ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa amefurahishwa na kitendo cha wanafunzi hao kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na hamasa ya mapambano dhidi ya rushwa kwenye jamii inayowazunguka.

Mhe. Mkuchika ameitaka klabu hiyo kuendelea kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuendelea kuliwezesha taifa kukusanya kodi inayowezesha shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
“Serikali inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa, na ndio maana imeongeza makusanyo ya kodi kwa mwezi toka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi trilioni 1.3 na kuongeza kuwa kitendo cha Serikali kununua ndege, kujenga barabara na kutoa elimu bure ni matokeo ya makusanyo hayo”, amefafanua Mhe. Mkuchika.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 Bw. Mzee Mkongea Ali, licha ya kufurahishwa na utendaji kazi wa klabu hiyo ya kupinga rushwa amewaeleza wanafunzi hao kuwa, Serikali haipo nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa ndio maana iliunda mahakama maalumu ya wahujumu uchumi na mafisadi ambayo imeshaanza kufanya kazi toka mwaka 2016 kwa kusikiliza kesi zipatazo1340 ambapo watuhumiwa 685 wamehukumiwa na wanatumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, vita dhidi ya rushwa si ya Serikali pekee hivyo ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kupitia vyombo vyake hususani Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanatoa taarifa zitakazowezesha vyombo hivyo kuwabaini wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo kwa kiasi kikubwa vinakwamisha maendeleo ya taifa.

Mhe. Mkuchika amepata fursa ya kupokea Mwenge wa Uhuru akiwa katika ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma wilayani Newala.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji Newala waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru mara baada ya ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2019 kuwasili katika halmashauri hiyo ya mji na kufanikiwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
 Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 Bw. Mzee Mkongea Ali akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji Newala waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru mara baada ya Mwenge huo kuwasili katika halmashauri hiyo ya mji huo na kufanikiwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akishiriki kuupokea Mwenge wa Uhuru ulipowasili katika Halmashauri ya Mji Newala.
 Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Mji Newala waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru mara baada ya ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2019 kuwasili katika halmashauri hiyo ya mji na kufanikiwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Mwenge wa Uhuru ukiwa mbele ya Zahanati ya Tupendane iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara baada ya ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2019 kuitembelea Halmashauri ya Mji Newala na  kukagua ujenzi wa jengo hilo ili kujiridhisha na ubora wa jengo ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha za Serikali zilizotolewa na Serikali kujenga zahanati hiyo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad