HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 30, 2019

KUFIKIA JUMATATU WANANCHI WA KISARAWE KUANZA KUPATA MAJI SAFI NA SALAMA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Kufikia mapema wiki ijayo, Wakazi wa mji mdogo wa Kisarawe wanaondoka na na adha ya maji ya muda mrefu baada ya ujenzi wa mradi wa Kisarawe kukamilika kwa asilimia 99.

Hatua hiyo imefikiwa, baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kukamilisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita Milioni 6 kukamilika.

Mradi huo wenye thamani ya Bilioni 10.6 uliojengwa kwa fedha za ndani za Dawasa unaotoa maji kutoka Tanki la maji la Kibamba hadi Kisarawe.

Kuanza kwa mradi huo kutawanufaisha wananchi wengi zaidi na maunganisho mapya 1000 watakaounganishwa maji kwa mkopo na kulipa ndani ya mwaka mmoja.

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameupongeza uongozi wa Dawasa kwa jitihada kubwa walizozifanya ndani ya muda mfupi kwa kuhakikisha maji yanafika katika mji mdogo wa Kisarawe.

"Naupongeza uongozi wa Dawasa, Mwenyekiti, Mkurugenzi na watendaji wengine kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha wanajenga mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Bilioni 10.6 kwa fedha za ndani na kuleta maji kwenye Mji mdogo wa Kisarawe,"

"Mradi huu umechukua muda mfupi sana, na ndani ya siku tatu hizi nataka kuhakikisha wananchi wanapata maji kesho nitaandamana na baadhi ya viongozi kuelekea Kibamba maji yanakoanzia ili kujionea mwenyewe," amesema Aweso.

Amesema, kuna changamoto ya umeme ambapo amewahakikishia wananchi wa Kisarawe mita itapatikana na maji yataanza kuingia kwenye tanki na huduma ya maji itaanza.

Kaimu Mkurugenzi Uwekezaji Miradi Dawasa Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema mradi wa maji Kisarawe umekamilika kwa asilimia 99 na kazi iliyobaki ni ndogo sana na Dawasa wanaendelea kuhakikisha ndani ya muda mfupi maji yanafika kama agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli alilolitoa.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Jokate Mwengelo amewataka wananchi wa mji mdogo wa Kisarawe kuwa na subira ndani ya siku chache wataanza kupata maji safi na salama.

" Niwatake na kuwaomba wananchi wa Kisarwe na wale walio nje ya mji huu kwamba kwa sasa nawakaribisha kuja kuwekeza kwenye Mji mdogo wa Kisarawe, maji yatakayokuwa hapa yanatosheleza mahitaji ya wakazi wote ambapo kwa sasa ni Lita Milion 1.2 zinazohitajika ila Dawasa wametuletea Lita Milion 6," amesema.

Mji mdogo wa Kisarawe unapata maji kutoka Mtambo wa Ruvu Juu na umeweza kufanikishwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ukitekelezwa na Dawasa ambapo kufikia Septemba Mwaka huu Mji huo umekabidhiwa rasmi kwa Mamlaka hiyo.

Mbali na mradi huo, Naibu ameweza pia kutembelea shule aliyosoma ya Pugu Sekondari, Shule aliyofundisha Kisarawe pamoja na Kisima alichokuwa anatumia kwa ajili ya matumizi ya maji sambamba na mradi wa maji wa Jet Buza wenye thamani ya Bilion 2 unaotarajia kuanza hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akipata maelezo ya miradi ya maji kwa Wilaya ya Ilala kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema baada ya kufika ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akisalimiana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pugu ambapo amewaahidi kero ya maji ya miaka mingi itafikia ukingoni baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Kisarawe hadi Pugu wenye thamani ya Bilion sita unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira. Aweso amesoma shule hiyo katika mchepuo wa Sayansi PCB na kuhitimu kidato cha sita mwaka 2007.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiwa amekaa kwenye dawati alilolitumia wakati anasoma kwenye shule ya sekondari Pugu mchepuo wa Sayansi PCB na kuhitimu kidato cha sita mwaka 2007.M
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akizungumzia maendeleo ya mradi wa maji wa Kisarawe unaotarajiwa kuanza kutoa huduma ya maji safi na majitaka kufikia Mwanzoni mwa Mwezi Novemba. Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametembelea mradi huo uliokamilika kwa asilimia 99.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa maji Kisarawe Kutoka DAWASA Mhandisi Ishmael Kakwezi na kuangalia matoleo mojawapo yaliyopo kwenye tanki la maji la Kisarawe linaloweza kuhifadhi maji Lita Milion 6 kwa siku.
Naibubu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akitembelea ujenzi wa mradi wa maji Kisarawe uliokamilika kwa asilimia 99, utakaohudumia wakazi wa Mji mdogo Kisarawe wenye thamani ya bilion 10.6 uliojengwa kwa fedha za ndani za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akionesha Kisima cha Mani alichokuwa anakitumia wakati anafundisha shule ya Msingi Kisarawe na bado kinaendelea kutumika na wananchi wa Kisarawe.
Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji Miradi DAWASA akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso baada ya kutembelea mradi wa Jet Buza utakaoanza Jeti na kulaza mabomba hadi Buza.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad