KILA PALIPO NA AMCOS PAWE NA SACCOS - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 11 October 2019

KILA PALIPO NA AMCOS PAWE NA SACCOS

Viongozi wa Vyama vya Akiba na Mikopo waliopata tuzo za vyama vyenye utendaji mzuri wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi (katikati) Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Prof. Alfred Sife pamoja na viongozi wa Sekta ya Ushirika, Jijini Arusha

Wanaushirika wa Vyama vya Akiba na Mikopo wameshauriwa kuanzisha vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) katika maeneo zilipo vyama vya Ushirika wa mazao (AMCOS) kwa madhumuni ya kuwezesha ununuzi na upatikanaji wa pembejeo za kilimo kama vile mbolea, mbegu na dawa za wadudu waharibifu wa mazao ili kukuza uchumi pamoja na Sekta ya Ushirika. Ushauri huo ukitokana na azma ya Serikali katika kuhakikisha Sekta ya kilimo inaendelea kukuwa na kuongeza mchango wa Pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Prof. Alfred Sife akifunga maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Kitaifa yaliyokuwa yakifanyika Jijini Arusha yaliyoandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT)

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo Prof. Sife ameongeza kwamba vyama vya Akiba na Mikopo ni chachu ya maendeleo katika Jamii kwani vyama hivyo vimekuwa msaada kwa wananchi wengi kutokana na upatikanaji wa mikopo yenye riba na masharti nafuu unaowawezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali kama vile kuboresha makazi, kupata mitaji ya biashara za aina mbalimbali.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bw.Tito Haule katika kufunga maadhimisho hayo alipata fursa ya kutoa wito kwa vyama vya Akiba na Mikopo kuendelea kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za Vyama vya Ushirika kwa mujibu wa Sheria Namba.6 ya Mwaka 2013 ili kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinaendelea kuwa salama na wanachama wanapata huduma bora. Aidha, Mrajis alipongeza jitihada za SCCULT katika kuunganisha, kuviweka pamoja na kuhamasisha vyama kuendelea kujiunga na Chama Kikuu hicho.

“Mafanikio katika uendeshaji na usimamizi wa vyama hivi ni dhahiri kwamba unatokana na mchango mkubwa wa utendaji wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Niwaombe wanaushirika tuendelee kushirikiana kwani Ushirika ni sauti ya pamoja, Chama cha Ushirika kinapata nguvu zaidi pale kinapoungana na vyama wenzake chini ya mwavuli wa Chama Kikuu cha Ushirika”
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) Dkt. Gervas Machimu alisema vyama vya Akiba na Mikopo hivi sasa vipo 6,137 nchini ambavyo vinapatikana nchini kote mijini na vijijini. Akifafanua zaidi kwamba SCCULT inaendelea kutoa msukumo wa vyama hivi hususan maeneo ya vijijini kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi, kuendeleza kilimo, uvuvi hasa wakati huu tunapoelekea uchumi wa viwanda. Mwenyekiti huyo alitoa rai kwa vyama kuendelea kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi, wanachama bila kusahau wajibu wa kujali jamii katika mazingira ya vyama hivyo.

Dkt. Gervas alibainisha baadhi ya changamoto zinazozikabili vyama hivyo ni pamoja na tozo za makato ya SACCOS wanazokatwa watumishi kupitia Hazina akiomba Serikali kuangalia namna bora ya kurejea suala hili ili kukuza na kuendeleza ndoto za wanachama wa vyama vya Akiba na Mikopo. Mwenyekiti alieleza baadhi ya taasisi kutowasilisha makato ya marejesho ya mikopo ya SACCOS kwa wakati kunarudisha nyuma dhamira njema ya kukua kiuchumi kwa vyama na wanachama kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti alisema SCCULT itaendelea kushirikiana kwa karibu na Vyama vya Akiba na Mikopo hivyo vyama vitumie fursa hiyo kupata ushauri, ufafanuzi, elimu na miongozo ya kuboresha utendaji wa vyama.
“Niwaombe wajumbe wa Bodi wa za Vyama vya Akiba na Mikopo, watendaji pamoja na wanachama kuendelea kushirikiana na chama chenu Kikuu cha SCCULT ili kuboresha utendaji wa vyama na kukuza Sekta ya Ushirika,”.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bi. Elizabeth Makwabe akitoa shukrani wakati wa kufunga maadhimisho hayo amesema Tume imejipanga na kujiimarisha zaidi katika kuendelea na uhamasishaji wa vyama vya Ushirika hususani kwa wanawake na vijana. Akiongeza kwamba Tume ina dhamira ya kuanzisha Jukwaa mahususi la wanawake katika Ushirika ili kuwahamasisha zaidi wanawake waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume akifafanua jambo kwa wanaushirika wakati wa kufunga maadhimisho kufunga maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Kitaifa, Jijini Arusha
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Prof. Alfred Sife akifunga rasmi maadhimisho ya ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Kitaifa, Jijini Arusha
Mwenyekiti wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Wanawake wa Karagwe mkoani Kagera Bi. Safina Amran akipokea Tuzo ya Chama chenye utendaji mzuri katika Sekta ya ushirika wa Akiba na Mikopo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad