HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 10, 2019

JAJI MKUU: SHERIA ITUMIKE IPASAVYO KUDAI TAARIFA

Na MISA Tanzania.

Ujumbe wa taasisi ya MISA Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Salome Kitomari umemtembelea na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo, Bi. Kitomari ameitambulisha MISATAN pamoja na kuelezea majukumu yake mbalimbali kwa Mhe. Jaji Mkuu ikiwemo kutetea na kufanya uzengezi kuhusu utoaji na upataji taarifa nchini.

Mwenyekiti wa MISA amezungumzia uhusiano mzuri uliopo baina ya taasisi yake na Mahakama ya Tanzania. Uhusiano huo umejikita ktk kuimarisha na kutetea haki ya utoaji na upatikanaji wa taarifa zenye maslahi kwa umma. “Katika hili, MISA kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania tumeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi zaidi ya 300 wa kada mbalimbali za Mahakama kuhusu namna bora ya kuwahudumia wateja na mbinu za utoaji wa taarifa kwaumma” alifafanua Bi. Kitomari.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na MISA Tanzania, mafunzo haya yameongeza weledi kwa washiriki na kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa taarifa za Mahakama hapa nchini. Aidha, Mwenyekiti wa MISA alisisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizi mbili
pamoja na kuhusisha taasisi nyingine za kihabari ili kupanua wigo wa utoaji na upatikanaji wa taarifa za kimahakama zenye maslahi ya umma.

Bi. Kitomari ameshauri kufanyika mikutano kati ya MISA TAN, Mahakama ya Tanzania na taasisi nyingine za Habari ili kuimarisha ushirikiano, imani na uwajibikaji katika mchakato mzima wa utoaji na upatikanaji wa taarifa kwa wananchi. Pia, ameshauri kuwepo kwa mafunzo endelevu ya huduma kwa mteja na upatikanaji wa taarifa kwa kuhusisha viongozi wa juu wa Mahakama wakiwemo Majaji, Mahakimu na afisa tawala.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania ameipa changamoto MISATAN na taasisi nyingine za Habari nchini kuitekeleza ipasavyo Sheria Namba 6 ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016 katika kudai taarifa zenye maslahi kwa umma na taifa. “Sheria hii inatoa shurti ya kutoa taarifa zinazotakiwa na umma, hivyo sio Fadhila bali ni amri. Hivyo ni vyema kuangalia ni kwa namna gani tunatumia sheria hii kushurutisha utoaji wa taarifa sahihi kwa wananchi” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Aliongeza kwamba ni wajibu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake kikamilifu katika kutekeleza sheria hii ipasavyo. “Kwa kufanya hivyo tutakua tumetekeleza takwa la Kikatiba na kisheria” amehimiza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Prof. Juma amevitaka vyombo vya Habari kuzingatia weledi katika kuhabarisha umma ili kuepusha mifarakano katika Jamii. Amewahimiza waandishi wa habari nchini kujikita zaidi katika kuandika habari za kiuchunguzi badala ya kutegemea habari za matukio. “Habari za kiuchunguzi huhusisha utafiti na ushahidi wa jambo. Kuripoti habari hizi kutapunguza malalamiko na mifarakano katika jamii” amehitimisha Mhe. Jaji Mkuu.</div>
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mwenyekiti wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari (hayupo pichani) pindi ujumbe kutoka Taasisi hiyo ulipomtembelea Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa MISATAN-Tanzania, Bi. Salome Kitomari akizungumza jambo na Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani). Mhe. Jaji Mkuu akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa kwanza kushoto ni Katibu wa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Adrian Kilimi, kulia ni Maafisa kutoka MISATAN na Mahakama. Maafisa kutoka MISATAN-Tanzania, (kushoto), Mwenyekiti, Bi. Salome Kitomari na Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema Kasabuliro kwa pamoja wakinukuu masuala yaliyokuwa yakitolewa na Mhe. Jaji Mkuu. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka MISATAN-Tanzania na baadhi ya Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika mazungumzo hayo, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari, wa pili kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa kwanza kushoto ni Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema Kasabuliro na wa kwanza kulia ni Salum Tawan, Mkutubi-Mahakama ya Tanzania. (Picha na Mary Gwera, Mahakama)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad