DKT. MPANGO: BENKI YA DUNIA IWEKEZE FEDHA KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI YA SERIKALI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 17 October 2019

DKT. MPANGO: BENKI YA DUNIA IWEKEZE FEDHA KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI YA SERIKALI

Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington Dc
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) ameiomba Benki ya Dunia-WB iwatume wataalam wake nchini Tanzania ili waainishe miradi mikubwa ya kimkakati inayotakiwa kutekelezwa kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP) badala ya taasisi hiyo ya Fedha Duniani kutaka Serikali itekeleze miradi midogo isiyo na tija kubwa kwa Taifa

Dkt. Mpango ametoa ushauri huo Mjini Washington DC nchini Marekani baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem ambapo aliwasilisha miradi mbalimbali ambayo Serikali inatekekeleza na ambayo ameiomba Benki hiyo isaidie rasilimali fedha.

‘’Nisingependa kuona Taasisi kubwa ya Kifedha kama Benki ya Dunia inakimbilia kufadhili utekelezaji wa vimiradi vidogo vya kujenga hostel au hotel za nyota tano; Kwa sasa nchi yetu inahitaji kujikita zaidi katika miradi mikubwa  ambayo itawaletea maendeleo ya haraka wananchi wetu’’ alisisitiza Mhe.Mpango.

Mhe. Mpango aliendelea kusisitiza kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa na inayohitaji fedha nyingi kuikamilisha, hivyo ni vyema Benki hiyo ikajielekeza katika kusaidia utekelezaji wa miradi hiyo. 

Dkt. Mpango alianisha miradi kama ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji mkoani Pwani, Mradi wa Ujenzi wa Reli kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay, Mchuchuma na Liganga ambako kuna rasilimali kubwa ya Madini ya Chuma na Makaa ya Mawe. 

Aidha Dkt. Mpango alisema katika kutekeleza vyema miradi ya PPP Serikali imejikita katika mambo mawili moja ni kuwa na programu ya kujenga uwezo kwa maana ya wataalamu wa kuitambua hiyo miradi lakini pia, kuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina ili kujenga uwezo wa majadiliano na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi hiyo.

‘’Nimewahimiza kwamba; kama kweli tunataka kutekeleza kwa ufanisi mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP) ni lazima tutekeleze miradi mikubwa, na kwa kuanzia, wangekuja kuanza kutekeleza ule mradi wa kujenga reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbaba-Bay, Mchuchuma hadi Liganga’’ alisema Mhe.Mpango.

Aliongeza kuwa ukamilishaji wa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuchochea kwa kasi maendeleo ya nchi  kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo inapopita reli hii.

Dkt. Mpango alimshukuru Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem kwa kukubali maombi mengi kutoka Tanzania ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango(katikati) akiwa na ujumbe wa Tanzania wakifuatilia majadiliano na Benki ya Dunia kwenye Mkutano uliofanyika Jijini Washington DC.
 Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird akichangia jambo kwenye kikao kati ya Benki ya Dunia na Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango (Mb) kwenye Mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia-WB na Shirika la Fedha la Kimataifa -IMF inayofanyika Jijini Washington nchini Marekani.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika, Nd.Hafez Ghanem akifuatilia majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Benki hiyo, Jijini Washington DC. Kulia kwa Nd.Hafez ni Mshauri Mwandamizi  Maendeleo Endelevu kwa  Afrika, Bw.Thomas O’Brien.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad