HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 3, 2019

DKT. KIJAJI AITAKA TRA KUONGEZA WIGO WA WALIPA KODI

Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kuandaa Mkakati mahsusi utakaosaidia kuongeza wigo wa walipa kodi nchini kutoka idadi ya zaidi ya walipa kodi milioni mbili nukta 7 (2.7m) waliosajiliwa na Mamlaka mpaka sasa.

Dkt. Kijaji aliyasema hayo alipofanya ziara ya kawaida ili kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo katika Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya Mkoa wa kikodi wa Kinondoni.

Mhe.Naibu Waziri alisema ili kuwaondolea mzigo walipa kodi waliopo sasa, jitihada za makusudi zinahitajika ili kuongeza idadi ya walipa kodi.

Dkt. Kijaji ameitaka TRA kuandaa mpango mkakati utakaoonyesha kuwa baada ya miaka miwili Mamlaka hiyo itakuwa imeongeza idadi ya walipa kodi zaidi ya milioni mbili,kwa kufanya hivyo Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania watakuwa wamejibu hoja iliyotolewa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaondolea mzigo walipa kodi waliopo sasa.

Aidha Mhe. Kijaji ameitaka TRA kumuandalia na kuwasilisha kwake takwimu ya ongezeko la walipa kodi lililotokana na zoezi la kugawa vitambulisho vya wajasiriamali nchini. 

“Lengo la kugawa vitambulisho hivyo lilikuwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi, hivyo ni vyema kujua tumeongeza walipa kodi wangapi waliotokana na zoezi hilo” alisisitiza Dkt. Kijaji

Kwa upande wa kodi ya majengo, Dkt. Kijaji ameitaka Mamalaka ya Mapato Tanzania kuhakikisha inapata orodha ya nyumba zote nchini kwa kuorodhesha wamiliki wa nyumba hizo na mawasiliano yao na kisha kuandaa kanzi data itakayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo. 

Dkt. Kijaji amesema ili kudhibiti upotevu mapato yanayotokana na kodi ya majengo ni lazima TRA wafanye kazi usiku na mchana kuhakikisha kanzidata ‘database’ hiyo inakamilika ambayo itatumika kuwakumbusha walipa kodi kupitia ujumbe mfupi wa simu ambapo itasaidia katika ukusanyaji wa kodi hiyo.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Meneja wa Mkoa wa kodi wa Kinondoni Bw. Massawe Masatu alisema kuwa pamoja na changamoto wanazopitia, Ofisi ya Mkoa wa kodi wa Kinondoni kwa mwaka 2018/19 ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 713ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 794, sawa na asilimia 86 ya lengo.

Mhe. Naibu Waziri aliwapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo na kuwataka kuwatumia vizuri watumishi hao katika kuongeza mapato ili kuwezesha Serikali kuwahudumia vyema wananchi. 

Dkt. Kijaji ameuagiza Uongozi wa Mamlaka hiyo kuwapa ushirikiano watumishi wanaofanya kazi zao kwa weledi, na kutosita kuwachukulia hatua wale wote watakaonekana wana nia ya kuirudisha nyuma Mamlaka hiyo.
 Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi wa Kinodoni Bw. Massawe Masatu, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi za Mamlaka hiyo katika mkoa wake kwa Mhe. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alipotembelea ofisi hiyo, Jijini Dar es Salaam.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akitoa maelekezo kwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kinondoni, Bw. Massawe Masatu wakati wa ziara yake aliyofanya katika ofisi hizo.
 Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango akitoa maagizo kwa Naibu Kamishina wa Mamalaka ya Mapato Tanzania, Nd. Albert Kingu wakati wa mkutano wake na viongozi wa Mamlaka hiyo wa Mkoa wa kodi wa Kinondoni.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kinondoni.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt.Ashatu Kijaji akisisitiza jambo kwa viongozi wa Ofisi ya Mkoa wa kodi wa Kinondoni wakati alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji akiwasikiliza walipa kodi waliokuwa wakisubiri kupatiwa huduma katika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo Millenium Tower, Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad